Katika kuelekea maadhimisho ya miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewezesha ujenzi wa bweni la watoto wa kike wenye mahitaji maalumu katika shule ya msingi Nansimo, iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mh. Dkt Vicent Anney siku ya tarehe 23/4/2024 alifanya ziara ya kutembelea na kukagua bweni hilo ili kuona hatua ilipofikia, katika ziara yake Mh. Mkuu wa Wilaya aliongozana na kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya, TARURA, TANESCO, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, pamoja na baadhi ya wakuu wa idara kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
Dkt Anney alisema, mradi huu unatakiwa uwe na tija kwa wananchi wote wa Kata ya Nansimo na maeneo ya jirani, kwani hii ni zawadi ya pekee aliyoitoa Mh. Rais katika maadhimisho haya ya miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo mnatakiwa muhakikishe mnausimamia vyema ili uweze kukamilika kwa wakati uliopangwa na kuwasaidia watoto wetu wenye mahitaji maalumu kuweza kupata elimu katika mazingira yaliyo rafiki.
Akisoma taarifa ya mradi wa ujenzi Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Nansimo, Bi. Jane Nsinwa alisema mradi huu unafadhiliwa na fedha kutoka serikali kuu, ambapo walipokea kiasi cha Tshs Million 128, na hadi sasa ujenzi ulipofikia wameshatumia kiasi cha Tshs Million 44,326,000/= na ujenzi upo hatua ya umwagaji wa jamvi, na unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2024.
Mkuu wa Wilaya alimpongeza Diwani wa Kata ya Nansimo, Mh. Edward Justas Namwatta, viongozi na wananchi wa kijiji cha Nansimo kwa usimamizi wao mzuri katika ujenzi wa mradi huo, hivyo aliwaagiza kuhakikisha wanawasimamia mafundi ili kuweza kukamilisha mradi kwa wakati.
“Mradi kwa ujumla unaendelea vizuri sana hadi hapa ulipofikia, ongezeni juhudi katika kuhakikisha mnawasimamia mafundi wote wanaojenga hapa ili kukamilisha kwa wakati, na hongereni sana.” Alisema Dkt. Anney.
Pia, alitembelea na kukagua ukamilishaji wa zahanati mbili zilizopokea kiasi cha Tshs Million 50 kila moja kutoka serikali kuu, ambazo ni zahanati ya Mwiseni na Nambaza. Katika zahanati ya Nambaza alipongeza kwa ujenzi mzuri unaoendelea na aliagiza kufanyika marekebisho kwa baadhi ya maeneo yaliyokuwa na changamoto na kuhakikisha mafundi wanamalizia ukamilishaji wa zahanati hiyo ili iweze kufunguliwa mapema na wananchi waweze kupata huduma ya Afya kwa ukaribu.
Kibara Stoo.
Anuani ya Posta: 126, Bunda
Simu: 0282621055
Hamishika: 0742163056
Barua Pepe: ded@bundadc.go.tz
Haki Miliki@ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda