Siku ya Wazee Duniani imeadhimishwa Wilayani Bunda katika Kijiji cha Neruma, Kata ya Neruma ambapo Wazee mbalimbali walipata fursa ya kukutana, kuburudika pamoja, kupata ujumbe uliobebwa na maadhimisho hayo na hatimaye kupokea vitambulisho vya matibabu bure kwa Wazee. Siku hii Duniani huadhimishwa tarehe 1/10/2017, wilayani Bunda siku hii iliadhimishwa tarehe 20/10/2017 ambapo mgeni rasmi alitakiwa kuwa Ndg. Lydia Bupilipili ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Bunda lakini kutokana na kuwa na majukumu mengine aliwakilishwa na Katibu Tawala Wilaya Ndg. Masalu Kisasila.
Kauli mbiu katika maadhimisho hayo ilikuwa ni: "Kuelekea Uchumi wa Viwanda: Tuthamini Mchango, Uzoefu na Ushiriki wa Wazee kwa Maendeleo ya Taifa".
Pamoja na mambo mengine, tukio muhimu kwenye maadhimisho hayo lilikuwa ni kuwakabidhi Wazee wapatao 235 vitambulisho vya matibabu bure. Lengo la Idara za Afya na Maendeleo/Ustawi wa Jamii ni kutoa jumla ya vitambulisho kwa Wazee 9,994 ifikapo Mwaka 2020.
Pia, mgeni rasmi aliyeongozana na Viongozi wengine akiwemo Mkurugenzi Mtendaji (W) Ndg. Amos Kusaja, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Mhe. Isack Maela alitumia fursa hiyo kutoa msisitizo wa Idara ya Afya kutenga Dirisha maalumu katika Vituo vya kutolea huduma za afya zikiwemo Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati ili kuboresha utoaji huduma kwa Wazee hao. Wauguzi nao walitakiwa kutumia lugha nzuri pale wanapowahudumia Wazee ambapo Wazee nao waliaswa kuendelea kuwa washauri wazuri wa Vijana ili kunusuru maadili ya Vijana na jamii kwa ujumla.
Kibara Stoo.
Anuani ya Posta: 126, Bunda
Simu: 0282621055
Hamishika: 0742163056
Barua Pepe: ded@bundadc.go.tz
Haki Miliki@ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda