KATIKA kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ukame unaosababisha upungufu wa chakula, Halmashauri ya Wilaya ya Bunda inakusudia kuanzisha mradi mkubwa wa kukabiliana na hali hiyo.
Mradi huo utakuwa na maeneo mbalimbali ikiwemo ufugaji wa samaki, kilimo cha kisasa cha mpunga, uboreshaji wa kilimo cha muhogo na alizeti na upandaji miti.
Akizungumza baada ya kutembelea maeneo yanayokusudiwa kutekelezwa mradi huo akiongozana na maofisa kutoka Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Ofisi ya Makamu wa Rais,afisa Mipango wa Halmashauri ya Bunda ambae pia Mratibu wa mradi huo, Dickson Balige alisema utakapokamilika utatoa faida mbalimbali ikiwemo uhakika wa chakula na faida za kiuchumi.
Balige alisema mradi huo umegawanyika katika sehemu nne ambazo ni ufugaji wa samaki wa vizimba na mabwawa, kilimo cha mpunga na mazao ya bustani, ambacho hakitatumia dawa.
Pia, alisema mradi huo utahusisha uboreshaji wa kilimo cha muhogo na alizeti na kwa upande wa mazingira kutakua na upandaji wa miti na uhifadhi wa vilima vipara na ufugaji wa nyuki.
Aidha, alisema kupitia mradi huo kutachimbwa visima virefu vya maji ambavyo pia vitanufaisha wananchi wanaozunguuka maeneo ya mradi.
“Mradi huu utachimba visima virefu na utafufua mradi wa maji ambao ulisimama kwa muda mrefu katika Kijiji Cha Isanju na Kasahunga. Tunataka njaa iishe kwa maeneo yote yatakayonufaika," alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya Bunda, Amos Kusaja alisema mradi huo utasaidia kuinua uchumi wa wanavijiji watakao vifikiwa na kuongeza mapato ya wilaya.
Alitoa rai kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano ili mradi huo uweze kufanikiwa.
Kwa upande wake Mratibu wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi kutoka NEMC, Fredrick Mulinda, alisema wametembelea maeneo yanayokusudiwa kujengwa mradi huo na kuridhika nayo kwa kuwa yanaendana na shughuli hiyo.
“Mradi huu utaleta manufaa kwa wananchi na kupunguza hali ya umasikini kwa wakazi wa vijijini Bunda unaochangiwa pia na mabadiliko ya tabianchi,” alisema.
MATUMAINI YA WENGI
Nyariho Chibara mkazi wa Kijiji cha Isanju, alisema endapo mradi huo utakamilika utakuwa na manufaa kwao kwa namna mbalimbali ikiwemo kutengeneza fursa ya kujipatia kipato.
“Tunaweza kuutumia kama chuo hasa kwa upande wa kilimo na ufugaji kisha na sisi kwenda kutekeleza miradi yetu kwa ngazi ya mtu mmoja mmoja,” alisema.
Janeti Paskali mkazi wa kijiji hicho alisema tatizo la upungufu wa chakula mara nyingi huwaathiri wanawake ambao ndio huishi muda mrefu na watoto na wanafamilia wengine wasio na uwezo wa kujitafutia, hivyo kupatikana kwa mradi utakaotoa uhakika wa chakula ni jambo la kushukuru.
Mradi huo unaotarajiwa kuanza utekelezwaji hivi karibuni utaghalimu sh. bilioni 3.2kwa udhamini wa Mfuko wa Maziangira Duniani.
Kibara Stoo.
Anuani ya Posta: 126, Bunda
Simu: 0282621055
Hamishika: 0742163056
Barua Pepe: ded@bundadc.go.tz
Haki Miliki@ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda