Baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Bunda likiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Mh. Charles Manumbu, siku ya tarehe 19/12/2024 walifanya ziara ya kutembelea Halmashauri ya Wilaya ya Geita.
Lengo kuu la ziara hiyo ni kujifunza namna ya ujenzi wa miundombinu imara na bora ya majengo, pamoja na ukusanyaji wa mapato ya ndani kupitia mialo ya samaki na dagaa.
Aidha, katika ziara hiyo, walitembelea na kukagua ubora wa jengo la kituo cha Afya cha Nkome kinachojengwa na kampuni ya mgodi wa dhahabu wa Geita kupitia fedha za (CSR),Ofisi ya kata Nzera ambayo imejengwa kwa fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri.
Pia, walitembelea mwalo wa dagaa uliopo kata ya Nkome na kuweza kujifunza namna wanavyokusanya ushuru kwa njia ya mashine (POs) , namna ya ujenzi wa vichanja vya kuanikia dagaa baada ya kuvuliwa ziwani, walitembelea mwalo wa kuvulia samaki aina ya Sangara na kujifunza jinsi wanavyokusanya mapato na namna wanavyosafirisha samaki baada ya kulipiwa ushuru
Waheshimiwa madiwani waliweza kuuliza maswali mbalimbali kutoka kwa wenyeji wao, na kupewa ufafanuzi wa yote waliyotaka kuyafahamu, pia walishukuru kwa ziara nzuri ya mafunzo na mapokezi mazuri waliyoyapata. Waliahidi kwenda kuboresha zaidi katika masuala ya ukusanyaji wa mapato kupitia vyanzo walivyo navyo sasa, ili waweze kuongeza zaidi mapato ya ndani ya Halmashauri.
Pia, waliwashukuru na kuwapongeza kwa ujenzi Bora na imara wa majengo yao.
Katika ziara hiyo, Waheshimiwa madiwani waliongozana na baadhi ya wakuu wa idara na vitengo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Bw. George S. Mbilinyi.
Kibara Stoo.
Anuani ya Posta: 126, Bunda
Simu: 0282621055
Hamishika: 0742163056
Barua Pepe: ded@bundadc.go.tz
Haki Miliki@ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda