
Halmashauri ya Wilaya ya Bunda siku ya tarehe 18/11/2025 imepokea viti na meza kutoka bank ya CRDB, kwa ajili ya shule mpya ya Sekondari Manchimweru iliyopo kata ya Mihingo.

Akizungumza katika makabidhiano hayo, meneja wa bank tawi la Bunda Ndugu Solomon Marwa alisema, Leo hii tumekuja hapa kwa ajili ya kukabidhi viti 40 na meza 40 vyenye thamani ya Tshs milioni 2 laki sita na elfu 70, katika shule ya Sekondari Manchimweru.

Naye, meneja mahusiano na Biashara za serikali Kanda ya ziwa, Bi. Huruma Gidiel alisema, bank ya CRDB imekuwa na utaratibu wa kutenga asilimia 1 Kila mwaka ya faida kwa ajili ya kurudisha katika jamii, na Leo hii tupo hapa kwa ajili ya kuwawezesha wanafunzi wa shule ya Sekondari Manchimweru kupata viti na meza hizi ili waweze kukaa katika mazingira mazuri wanapokuwa darasani.

Ndugu Lusingi Sitta, ambaye ni meneja wa bank ya CRDB Kanda ya ziwa, alisema tunao miradi unaoitwa " Keti jifunze" ambao tumekuwa tukishirikiana na shule mbalimbali katika kuhakikisha katika asilimia 1 ya faida tunayotenga tunaipeleka katika kusaidia madawati shuleni ili wanafunzi wetu waweze kukaa katika mazingira mazuri na rafiki wawapo darasani na shuleni.

" Tupo pamoja katika upande wa maendeleo na ninawahakikishia kwamba sisi CRDB tutailea shule hii na pia tunawashukuru sana kwa kuwa na akaunti katika benki yetu." Alisema Ndugu Sitta.

Ndugu Sitta aliwasisitiza wanafunzi hao kuhakikisha wanasoma vizuri sababu wamewawezesha mazingira mazuri ya kujifunzia, pia, niwashukuru wazazi kwa kuweza kusimamia ujenzi wa shule hii hadi kukamilika kwake.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Ndugu George S Mbilinyi, aliwashukuru bank ya CRDB kwa kushirikiana kwa pamoja katika kuhakikisha wanasaidiana katika kuleta maendeleo katika sekta ya elimu.

" Ninawaahidi, tutaendelea kushirikiana kwa pamoja katika kuhakikisha tunaleta maendeleo ya pamoja." Alisema Ndugu Mbilinyi.

Aidha, Mkurugenzi Mbilinyi, aliwasisitiza wanafunzi kuhakikisha wanavitunza viti na meza walizopokea wakati wote ili viweze kudumu kwa muda mrefu, tuendelee kushirikiana katika kuhakikisha tunakuza maendeleo.

Kibara Stoo.
Anuani ya Posta: 126, Bunda
Simu: 0282621055
Hamishika:
Barua Pepe: ded@bundadc.go.tz
Haki Miliki@ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda