Halmashauri ya Wilaya ya Bunda imekabidhi hundi ya zaidi ya Tsh. milioni 180 kwa vikundi 34 vya wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa makundi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu siku ya tarehe 31/12/2024 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
Akizungumza na wanufaika wa mikopo hiyo wakati wa kukabidhi hundi,kaimu Mkuu wa Wilaya ya Bunda Mhe, Meja Edward Gowele ambaye pia alikuwa mgeni rasmi, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kwa kutekeleza agizo la Mh. Raisi Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa mikopo hiyo ya asilimia 10 itakayosaidia kuongeza mapato ya Halmashauri.
Aidha, amewasisitiza wanufaika wa mikopo hiyo kutumia vyema fedha hizo kwa kuzingatia malengo ya kikundi na kujenga uchumi wa Halmashauri na familia zao kama ilivyo azma ya serikali ya kuwainua wananchi kiuchumi.
.“Ni lazima kurejesha fedha hizo kama kikundi na uaminifu utawasaidia kuendelea kupata mikopo zaidi na kutoa fursa kwa vikundi vingine ambavyo havijakidhi vigezo vya kupata mikopo hii, ili kuweza kupewa mikopo hiyo kwa awamu nyingine.” Amesema Mhe.Gowele
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Bw. George S.Mbilinyi amewataka wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 kutumia fedha hizo kuwanufaisha katika biashara zao na kuwainua kiuchumi huku akiwasisitiza kurejesha mikopo hiyo kwa wakati.
“Dawa ya mkopo ni kulipa hakikisheni mnalipa kwa wakati mikopo hiyo ilikuweza kupata nafasi ya kupata mikopo zaidi.”amesema Mbilinyi
Nao baadhi ya wanufaika wa mikopo hiyo ya asilimia 10 wameishukuru serikali ya awamu ya sita (6) kwa kutoa mikopo hiyo na kuahidi kutumia fedha hizo kujiinua kiuchumi kwa kufanya biashara zenye tija ili kuweza kurejesha mikopo hiyo kwa wakati sahihi.
Kibara Stoo.
Anuani ya Posta: 126, Bunda
Simu: 0282621055
Hamishika: 0742163056
Barua Pepe: ded@bundadc.go.tz
Haki Miliki@ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda