Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Bunda (BUWSSA), siku ya tarehe 06/01/2025 imetambulisha mradi wa maji kutoka Butiama hadi Nyamuswa, kwa wananchi wa Kata za Nyamuswa na Ketare, zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
BUWSSA imetambulisha mradi huo kwenye mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Bunda Mh. Boniphace Getere, wakati alipokuwa akisikiliza na kutatua changamoto za wananchi wa Kata ya Nyamuswa.
Mkurugenzi Mtendaji wa BUWSSA, Bi. Esther Gilyoma amesema Serikali ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya maji inatekeleza mradi wa kusambaza maji kupitia chanzo cha maji ya ziwa Viktoria.
" Utekelezaji wa mradi huo, unatarajia kuanza tarehe 01/02/2025 na kukamilika tarehe 30/01/2026, kwa gharama ya Tshs Bill 8.3 fedha kutoka Serikali kuu na utatekelezwa na Wakandarasi wawili ambao ni MOLI OIL MILLS pamoja, na GAT ENGINEERING CO. LIMITED". Alisema Bi. Gilyoma.
Mkurugenzi Mtendaji wa BUWSSA amesema, vijiji vitakavyo nufaika na mradi huo katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ni vijiji vitano (5), ambavyo ni kijiji cha Bukama, Makongo A, Makongoro B, Nyamuswa na Tiring'ati.
Naye, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Ndugu Stafa Nashoni, aliwashukuru na kuwapongeza BUWSSA katika usimamizi wa mradi huo na aliahidi kuwapa ushirikiano wa kutosha katika kuhakikisha wanatekeleza na kuukamilisha mradi huo kwa wakati ili wananchi wa Nyamuswa na Ketare waweze kupata maji safi na salama.
Pia, alimshukuru na kumpongeza Mh. Getere kwa kuandaa na kufanya mkutano wa hadhara kwa wananchi wa Jimbo la Bunda akiwa na lengo la kusikiliza na kutatua kero za wananchi wake.
Aidha, Ndugu Nashoni alimpongeza na kumshukuru Mh. Mbunge kwa kuweza kusimamia na kuhakikisha mradi huu wa maji kutoka Ziwa Viktoria unaletwa katika Kata za Nyamuswa na Ketare, ili wananchi waweze kupata maji safi na salama.
Mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kupitia Wilaya ya Butiama hadi Nyamuswa unasimamiwa na Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Bunda (BUWSSA), chini ya Mkurugenzi Mtendaji wa BUWSSA.
Kibara Stoo.
Anuani ya Posta: 126, Bunda
Simu: 0282621055
Hamishika: 0742163056
Barua Pepe: ded@bundadc.go.tz
Haki Miliki@ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda