Walimu Wakuu wa shule za msingi na Maafisa Elimu Kata wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda siku ya tarehe 10/11/2023 walipewa mafunzo ya kusimamia miradi mbalimbali ya maendeleo iliyopo katika Kata zao. Mafunzo hayo yalitolewa na Afisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Bw. Sayi Galan kwa kuwataka kufuata sheria na taratibu katika kuhakikisha wanaisimamia miradi yao vizuri.
Bw. Galan alisema kuna hatua mbili na muhimu za kufuata mara tu unapokuwa umepokea fedha kwa ajili ya Ujenzi wa mradi wowote katika shule, miradi hiyo ni kama Ujenzi wa madarasa, ofisi za walimu, nyumba za walimu na Vyoo, hii yote ni miradi ambayo ni lazima kuishirikisha jamii inayokuzunguka.
Hatua ya kwanza ni uendeshaji wa miradi, ambapo aliwaambia Walimu Wakuu na Maafisa Elimu Kata, kuhakikisha wanautambulisha mradi wowote kwa jamii, pindi wanapokuwa wameshapokea fedha za mradi kwa kuhakikisha taarifa zinafika kwa jamii kwa kufuata kanuni na taratibu, ikiwemo kuandika barua katika serikali ya kijiji na Kata na kuhakikisha mkutano wa hadhara unafanyika na Wanakijiji wa eneo husika wanatambulishwa kuanzia kiasi cha fedha walichopokea na aina ya mradi.
Pia, kuunda kamati kwa ajili ya kusimamia huo mradi ikiwemo kuwaaambia majukumu yao ni yapi, na kama kuna malipo yoyote ambayo itapata ni vyema kamati wakajulishwa mapema, kuliko kupelekea kukwama kwa mradi.
“Kuhakikisha mnatunza nyaraka zote za manunuzi vizuri kuanzia mwanzo wa mradi hadi kukamilika kwake, halafu kuhakikisha manunuzi yote yanafanyika kwenye mfumo, hivyo, aliwaambia, mnapopata fedha hizi za mradi ni lazima umshirikishe Mkuu wako wa Idara ambaye ndio mwenye uwezo wa kuingia kwenye huo mfumo na kufanya manunuzi, kinyume na hapo ni kukiuka wa taratibu na sheria za manunuzi.” Alisema Bw. Galan.
Afisa Mipango alisema, hatua ya pili ni Andiko la mradi, Mwalimu Mkuu unapopata fedha yoyote ya mradi ni lazima uandike Andiko la mradi huo na kuhakikisha unalifikisha katika ofisi ya Mipango iliyopo makao makuu ya Halmashauri, Andiko hilo linatakiwa kufuata kanuni na taratibu za uandishi kwa kuonyesha kiasi cha fedha ulichopokea, aina ya mradi unaoenda kuutekeleza, kuanza kwake hadi kukamilika kwake.
Naye, Kaimu Afisa Elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Bw. Phinius Ouko aliwaambia, Walimu Wakuu na Maafisa Elimu Kata wahakikishe pindi wanapotaka kuanza mradi wowote ule wahakikishe kwanza wanamueleza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, ili aweze kuwapatia Mtaalamu wa Ujenzi wa kuweza kuwaonyesha eneo sahihi kwa ajili ya ujenzi na kuwapatia ramani yenye kufuata vipimo sahihi na sio kujiamulia kujijengea kimya kimya pasipo kumshirikisha Mkurugenzi Mtendaji na kupelekea kujenga majengo yasiyofuata vipimo na yasiyokuwa na ramani.
Walimu Wakuu na Maafisa Elimu Kata walishukuru kwa elimu waliyopewa na kuomba elimu hiyo iendelee kutolewa mara kwa mara kwani wamekuwa wakipitia changamoto mbalimbali kutokana na kukosekana kwa elimu ya usimamizi na uendeshaji wa miradi ya serikali.
Mafunzo hayo yalihudhuriwa na Walimu Wakuu 16 pamoja na Maafisa Elimu Kata 6 kutoka katika Kata mbalimbali zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
Kibara Stoo.
Anuani ya Posta: 126, Bunda
Simu: 0282621055
Hamishika: 0742163056
Barua Pepe: ded@bundadc.go.tz
Haki Miliki@ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda