Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba nchini Tanzania (TMDA), siku ya tarehe 26/8/2025 walitoa mafunzo kwa watumishi wa AFYA katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
Akitoa mafunzo hayo, Mchunguzi Sehemu ya Ufuatiliaji Usalama wa Vifaa Tiba na Vitendanishi, kutoka TMDA Makao Makuu, Bi. Amina Kingo alisema, lengo la mafunzo hayo ni kuwapatia elimu watoa huduma ya afya na kuhamasisha utoaji wa taarifa za madhara na matukio yatokanayo na matumizi ya vifaa tiba na vitendanishi katika vituo vya kutolea huduma ya afya.
Bi. Kingo aliwaeleza umuhimu wa kutoa taarifa hizo na namna Mamlaka inafanya ufuatiliaji na uchunguzi ili ichukue hatua za kiudhibiti na kuzuia madhara hayo yasiendelee kutokea maeneo mengine ikiwa ni pamoja na kuviondoa vifaa tiba na vitendanishi vinavyobainika kuwa na ubora duni katika soko.
Pia, walifundishwa namna ufuatiliaji na uchunguzi wa vifaa tiba na vitendanishi unaofanywa na watengenezaji ili marekebisho yafanyike na madhara yasiendelee kutokea tena.
Bi. Kingo alisema madhara yanayotokana na matumizi ya kifaa tiba kisicho na ubora huwa ni makubwa zaidi pale yasipodhibitiwa mapema. Hivyo, kama wataalam wa afya, pale wanapobaini vifaa tiba au vitendanishi sio salama na havina ubora, ni vyema kutoa taarifa kwa usahihi na mapema ili viweze kudhibitiwa kabla madhara makubwa zaidi hayajatokea kwa watumiaji na wagonjwa.
Watumishi wa AFYA walitakiwa kuhakikisha wanatoa taarifa zilizo sahihi kuhusiana na vifaa tiba hivyo na kwa wakati ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa mapema na kusaidia kuboresha utoaji wa huduma na matibabu yaliyosahihi.
Naye, Mkaguzi wa Dawa na Vifaa Tiba kutoka ofisi ya TMDA, Kanda ya Ziwa Mashariki - Mwanza, Ndg. Kapilya Haruni aliwafundisha njia mbalimbali za utoaji taarifa zikiwemo fomu maalum ya rangi ya chungwa ambayo inatumika na namna ya kuzijaza fomu hizo.
Pia, walifundishwa njia nyinngine za kutoa taarifa kwa kutumia simu kwa kupiga bila malipo na ya ujumbe kupitia USSD Code: ambayo ni *152*00# ambayo ni bure kabisa, na kwa kutumia Portal ya mamlaka.
Kibara Stoo.
Anuani ya Posta: 126, Bunda
Simu: 0282621055
Hamishika:
Barua Pepe: ded@bundadc.go.tz
Haki Miliki@ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda