Mwenyekiti wa baraza la biashara ambaye pia, ni mkuu wa wilaya ya Bunda Mh. Dr. Vicent Anney akifungua kikao cha baraza la biashara siku ya tarehe 20/9/2023 kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya Bunda Mji.
Lengo la kikao hicho ni kujadili fursa za uwekezaji na uchumi katika halmashauri ya wilaya ya Bunda.
Mh. Dr. Anney aliwakaribisha wafanyabiashara mbalimbali kutoka wilaya ya Bunda waliohudhuria katika kikao hicho kuweza kujadili fursa mbalimbali za uwekezaji katika sekta ya kiuchumi na kilimo.
Mkuu wa Idara ya viwanda, biashara na uwekezaji kutoka halmashauri ya wilaya ya Bunda Bw. Samweli Werema alisema, wananchi wa halmashauri ya wilaya ya Bunda wanajishughulisha na kilimo, ufugaji na uvuvi ambao ni zaidi ya 80% na 20% wanajishughulisha na biashara na ujasiriamali, uchimbaji wa madini pamoja na uzalishaji viwandani.
Bw. Werema alisema, kutokana na halmashauri ya wilaya ya Bunda kwa ofisi na watumishi kuhamia Kibara kuna fursa nyingi za biashara kama huduma za vyakula, nyumba za kulala wageni na kupangisha, aidha, kuna fursa za biashara za vifaa vya ujenzi, vya ofisini na majumbani kwa uwepo wa miradi ya ujenzi na miundo mbinu ya elimu na afya toka serikali kuu.
“Kuna fursa za ujenzi wa kituo cha mabasi Kibara na kituo cha Mafuta kwa makubaliano na halmashauri ya wilaya, hizi ni fursa kubwa kwa uwepo wa magari mengi ya biashara na barabara za lami kutoka Musoma, Tarime, Serengeti, Mwanza, Simiyu kupitia Bunda kwenda Kibara, pamoja na barabara zinazopitika kutoka Ukerewe na Majita kwenda Kibara. Uwepo wa magari mengi ya halmashauri ya wilaya ya Bunda na magari mengine toka taasisi zingine na magari binafsi ni fursa kwa kituo cha Mafuta kitakachojengwa Kibara.” Alisema Bw. Werema.
Naye, Afisa kilimo wa halamashauri ya wilaya ya Bunda Bi. Balisimaki Shija alielezea umuhimu wa zao la mtama kama likitumika vizuri litasaidia kwa kiasi kikubwa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na pia katika kukabiliana na upungufu wa chakula kwa wakazi wa wilaya ya Bunda.
“Tangu mwanzo zao la mtama ndio zao kongwe kulimwa na kutumika kwa wingi wilayani Bunda likifuatiwa na ulezi, muhogo na viazi vitamu.” Alisema bi. Shija.
Mwenyekiti wa baraza la biashara Mh. Dr. Vicent Anney aliwashauri wataalamu watumie zaidi teknolojia za kisasa katika kilimo na Maafisa biashara kuwasilisha taarifa zao kwa takwimu zilizosahihi ili kuwavutia wawekezaji katika sekta ya biashara na kilimo kwa kutambua ni maeneo gani mazuri zaidi yanafaa katika uwekezaji.
Akihitimisha kikao hicho, Mh. Dr. Anney aliazimia mpaka mwakani halmashauri ianzishe uuzaji wa mazao kupitia stakabadhi ghalani hasa kwa mazao ya pamba na dengu ili kuwarahisishia wakulima kuuza mazao yao kwa bei iliyo halali badala ya kulanguliwa na wafanyabiashara kutoka shambani.
Kibara Stoo.
Anuani ya Posta: 126, Bunda
Simu: 0282621055
Hamishika: 0754335739
Barua Pepe: ded@bundadc.go.tz
Haki Miliki@ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda