Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Bunda, Bi. Changwa M. Mkwazu siku ya tarehe 4/10/2023 alipokea taarifa ya makabidhiano ya uratibu wa mradi wa kuhimili Athari za mabadiliko ya Tabianchi yaliyofanyika katika ofisi ya Mkurugenzi. Makabidhiano hayo yalifanyika baina ya ndugu Dickson Balige na ndugu Johanes Bucha.
Aliyekuwa Mratibu wa mradi ambaye anamaliza muda wake Ndugu Dickson Balige wakatika akikabidhi taarifa hiyo alisema, katika kipindi cha robo ya kwanza ya utekelezaji wa mradi, shughuli mbalimbali zimeanza kutekelezwa katika sekta ya maji, kilimo, ufugaji wa samaki na mazingira.
“Katika kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi mradi umeanza kusambaza maji kwa jamii kwa kuongeza mtandao wa maji katika vijiji vya Mumagunga na Muranda, kuanzisha na kuimarisha jumuiya za watumia maji (CBWOSOs) katika vijiji vya Muranda, Mwiruma, Mumagunga na Kibara”. Alisema Ndugu Balige.
Pia kwa upande wa kilimo mradi umelenga kuboresha maisha ya wakulima walioathiriwa na mabadiliko ya Tabianchi kwa kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula kwa kutumia kilimo kinachozingatia hifadhi ya mazingira.
“Kwa upande wa ufugaji wa samaki mradi huu umelenga kuhamasisha uvuvi endelevu katika halmashauri kwa kuanzisha ufugaji wa samaki kupitia mabwawa na vizimba katika vikundi vya ufugaji wa samaki ili kuboresha maisha na kuhimili athari za mabadiliko ya Tabianchi katika vijiji vya Mchigondo na Isanju. Kupitia mradi huu tumeweza kununua mitumbwi miwili na injini mbili za HP-15 kwa ajili ya utoaji wa huduma katika vizimba vya kufugia samaki”. Alisema aliyekuwa Mratibu wa mradi.
Ndugu Balige alisema, katika kuboresha mazingira na ikolojia kwa kuzingatia shughuli zinazoimarisha maisha ya jamii za vijiji vilivyoathiriwa na mabadiliko ya Tabianchi, kwa kuanzisha kitalu na upandaji wa miti katika vilima vipara vya Kata za Iramba, Neruma, Namhula, Chitengule na Igundu. Kupitia mradi huu tuliweza kupanda miche 159,030, ambapo miche 63,500 imepandwa katika taasisi mbalimbali za serikali na binafsi na miche 95,530 inaendelea kukuzwa katika kitalu.
Halmashauri iliandika kiushindani andiko la mradi huu ambao ulikidhi vigezo na kupitishwa na bodi ya mfuko wa mazingira duniani mnamo mwezi April, 2021 likiwa na thamani ya dola za Kimarekani 1,400,000.00 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za mradi kwa kipindi cha miaka mitatu.
Kibara Stoo.
Anuani ya Posta: 126, Bunda
Simu: 0282621055
Hamishika: 0742163056
Barua Pepe: ded@bundadc.go.tz
Haki Miliki@ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda