Katibu Tawala wa Wilaya ya Bunda Ndugu Salum Khalfan Mtelela kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Bunda Mh.Dkt Vincent Anney, siku ya tarehe 8/1/2025 amezindua rasmi bodi ya Afya ya Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, ambayo itaongoza kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo.
Katibu wa bodi ya Afya, ambaye ni Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Dkt. Hamidu Adinani alisema lengo la kuundwa kwa bodi ya Afya ni kwa ajili ya kusimamia huduma zote za Afya kwa kuhakikisha watoa huduma ya Afya kuanzia ngazi za vituo, na hospitali wanatekeleza majumu yao kwa kufuata kanuni, taratibu na Sheria za utendaji kazi, ili kupunguza na kuondoa changamoto mbalimbali ambazo jamii inakabiliana nazo kwa upande wa huduma ya Afya.
Dkt Adinani alisema, jukumu kubwa la bodi ya Afya ni kuhakikisha wanasimamia na kuhakikisha huduma za Afya zinaboreshwa kwa kuwahamasisha na kuelimisha jamii kujiunga na huduma za bima ya Afya ili waweze kupunguza gharama za matibabu pale wanapoenda katika vituo vya Afya na hospitali kwa ajili ya kupata huduma.
" Kusimamia bodi za Afya ndogo, ambazo zipo katika vituo vya Afya kwa kuhakikisha zinatekeleza majukumu yao ipasavyo, kusimamia mapato ya vituo vya Afya kwa kuhakikisha yanakusanywa kwa usahihi, kuwashauri mama wajawazito kujiunga na huduma ya M- mama kwa ajili ya kupata huduma ya haraka kwa kupiga namba ya simu Bure ya 115." Alisema Dkt Adinani.
Aidha, Ndugu Mtelela ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa bodi alisema, dhima ya bodi hii ni kuhakikisha inasimamia huduma ya Afya katika Halmashauri na kuhakikisha zinaboreshwa ili wananchi waweze kuhudumiwa vizuri.
" Tuhakikishe tunawasimamia vyema wahudumu wetu wa Afya, ili kuhakikisha wanatimiza majukumu yao kwa umakini kwa kufuata Sheria, kanuni na taratibu za taaluma zao. Tukahamasishe wananchi ili waweze kujiunga na huduma ya bima ya Afya ya iCHF, tukatimize majukumu yetu kama muongozo wa bodi ya Afya unavoelekeza, tufanye kazi kwa umoja na ushirikiano ili kuhakikisha bodi hii inatimiza malengo yake kwa kuhakikisha huduma za Afya katika Halmashauri zinaboreshwa." Alisema Ndugu Mtelela.
Katika uzinduzi wa bodi wajumbe walifanya uchaguzi wa kumchagua Mwenyekiti ambaye ataongoza kwa kipindi cha miaka mitatu, na uchaguzi ulifanyika kwa wajumbe kupiga kura na kumchagua Bi. Immaculata Maina kuwa Mwenyekiti wa bodi ya Afya ya Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
Kibara Stoo.
Anuani ya Posta: 126, Bunda
Simu: 0282621055
Hamishika: 0742163056
Barua Pepe: ded@bundadc.go.tz
Haki Miliki@ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda