Divisheni ya elimu ya Awali na Msingi ya Halmashauri ya Wilaya ya Bunda wamefanya kikao kazi cha tathimini ya Mtihani wa kumaliza elimu ya msingi darasa la saba (PSLE) na mitihani ya upimaji wa darasa la nne kwa mwaka 2024.
Kikao hicho kimefanyika siku ya tarehe 28/02/2025 katika ukumbi wa Chuo cha Ualimu Bunda, lengo kuu likiwa ni kujitathimini kiutendaji na kupanga namna sahihi ya mapinduzi ya elimu baada ya Halmashauri kushuka kwa asilimia 1.7 ikilinganishwa na matokeo ya mwaka 2023.
Akiwasilisha taarifa za matokeo ya darasa la saba kwa mwaka 2024 Afisa taaluma wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Bi. Restituta Malima amesema jumla ya wanafunzi 7851 walisajiliwa kufanya mtihani wa darasa la saba waliofanya mtihani ni wanafunzi 7157 sawa na asilimia 1.7 na kati yao waliofaulu ni 5,390 na kupelekea Halmashauri kuwa na ufaulu wa asilimia 76.
Akizungumza, Afisa Elimu ya Awali na Msingi Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Bw.Deusdedith Bimbalirwa amewataka walimu wakuu wa shule za msingi kutumia muda mwingi katika vituo vyao vya kazi ili kufuatilia ufundishaji wa walimu na ufaulu wa wanafunzi.
"Walimu wakuu mmekuwa mkitumia muda mwingi kufuatilia mambo ya kiofisi kuliko kuhudhuria katika vituo vyenu vya kazi, hivyo basi niwaombe majukumu hayo ya ufuatiliaji wa taarifa za kiofisi wakabidhiwe wahasibu na walimu wengine na badalayake nyie mshinde katika vituo vyenu vya kazi ili kufuatilia zaidi ufaulu wa wanafunzi."Amesema Afisa Elimu
Kwa upande wake Mdhibiti ubora wa shule Ndugu Anthony Kazungu amesema miongoni mwa sababu zinazopelekea kushuka kwa ufaulu ni pamoja na walimu kutumia mbinu za kufundishia zilizopitwa na wakati, utoro wa walimu na wanafunzi pamoja na walimu wakuu kuwa na migogoro na walimu wengine.
Aidha, amewataka walimu kujitambua kwa kuzingatia kiwango cha ufundishaji wanapokuwa darasani na kuongeza maarifa kutoka katika vyanzo mbalimbali ikiwemo vitabu.
Naye, mwakilishi wa Katibu tume ya walimu Ndugu,Charles Bisasaba amewataka walimu kuwa mfano bora na kujiepusha na tabia za ajabu ikiwemo mavazi yasiyofaa, utoro kazini, uchelewaji na migogoro midogomidogo huku akiwasisitiza kuwa miongoni mwa tabia ambazo hazitafumbiwa macho ni pamoja na mahusiano ya kimapenzi kati ya walimu na wanafunzi.
Hata hivyo walio hudhuria katika kikao hicho ni Afisa elimu Awali na Msingi,Afisa taaluma Awali na Msingi,maafisa elimu kata pamoja na walimu wakuu wa shule za msingi.
Kibara Stoo.
Anuani ya Posta: 126, Bunda
Simu: 0282621055
Hamishika: 0742163056
Barua Pepe: ded@bundadc.go.tz
Haki Miliki@ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda