Naibu Waiziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, Mhe. Anjelina Mabula (MB) ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kuandaa Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi. Agizo hilo limetolewa katika kikao kilichofanyika tarehe 22/2/2018 kikiwahusisha wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Mweyekiti wa Halmashauri pamoja na watumishi wa Idara ya Ardhi na Maliasili.
Akipokea taarifa ya Idara ya Ardhi na Maliasili iliyowasilishwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Bw. Martine Nkwabi, Mhe. Waziri aliweza kubaini kuwa Halmashauri haijafanya jitihada zozote za kuandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi ikiwa ni pamoja na kufanya upimaji wa maeneo ya Taasisi za Serikali. Hivyo basi, Mhe. Waziri alitoa agizo alilotaka litekelezwe mara moja. “Inasikitisha sana kuona kunakuwepo na migogoro ya ardhi katika vijiji vyetu. Kwa kiasi kikubwa migogogoro hii inasababishwa na kutokuwepo kwa mpango wa matumizi bora ya ardhi. Sasa ninawaagiza muandae mpango huo angalau kwa kuhusisha vijiji 5 vyenye migogoro ya ardhi na upimaji wa maeneo ya Taasisi za Serikali uanze kufanyika haraka iwezekanavyo”.
Pamoja na kuiagiza Halmashauri kuandaa mpango huo, pia ameutaka uongozi wa Halmashauri kuhakikisha kuwa migogoro yote ya ardhi haitatuliwi ofisini. Badala yake uwekwe utaratibu wa watumishi wa ardhi kutembelea maeneo yenye migogoro ya ardhi na kutatua migogoro hiyo hukohuko kwa kuzihusisha pande zote zenye mgogoro.
Awali akitoa taarifa ya Idara ya Ardhi na Maliasili, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Bw. Martine Nkwabi alimueleza Mhe. Waziri kuwa miongoni mwa changamoto kubwa zinazoikabili Idara ya Ardhi na Maliasili ni pamoja na uhaba mkubwa wa wataalamu na Usafiri katika Kitengo cha Ardhi. Bw. Nkwabi alibainisha kuwa Idara inayo mahitaji ya watumishi 10 lakini mtumishi aliyepo ni 1 tu na mtumishi huyo anatarajia kustaafu kwa mujibu wa sheria mwezi Juni mwaka 2018. Upungufu huu unachangia kwa kiasi kikubwa Idara kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa wakati na kwa ufanisi.
Akihitimisha kikao hicho, Mhe. Waziri alikiri kupokea changamoto hizo na kuahidi kuzifanyia kazi. Aidha alisisitiza matumizi sahihi ya mfumo wa ukusanyaji wa mapato kupitia tozo mbalimbali za ardhi. Mwisho alihimiza utoaji wa hati za viwanja kwa wakati ili kuepuka malalamiko ya wananchi yasiyokuwa ya lazima kwa kumtaka Afisa Ardhi Mteule wa Wilaya ya Bunda Bw. Baraka Kambira kuhakikisha kuwa anakamilisha taratibu za upatikanaji wa hati kwa wananchi walioomba kupewa hati tangu mwaka 2016 ndani ya siku saba. Kinyume na hapo uteuzi wa Afisa Ardhi Mteule utenguliwe mara moja.
Kibara Stoo.
Anuani ya Posta: 126, Bunda
Simu: 0282621055
Hamishika: 0742163056
Barua Pepe: ded@bundadc.go.tz
Haki Miliki@ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda