Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira iliipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kwa kukamilisha Ujenzi wa Josho la kuogeshea Mifugo lililopo katika Kijiji cha Chingurubila, Kata ya Namuhula.
Pongezi hizo zilitolewa wakati kamati ilipofanya ziara ya siku moja ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya Maendeleo siku ya tarehe 17/10/2023.
Miradi waliyotembelea na kukagua ni Josho la kuogeshea mifugo lililopo katika Kijiji cha Chingurubila, Kata ya Namuhula na kiwanja kilichotolewa na wananchi wa kijiji cha Mariwanda, Kata ya Hunyari kwa ajili ya ujenzi wa shule.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Bw. Oscar Jeremiah Nchemwa alisema, Josho hili limegharimu kiasi cha Tshs Millioni 23 kutoka serikali kuu hadi kukamilika kwake ila bado halijaanza kutumika sababu ya kusubiria uchanganywaji wa dawa kwa ajili ya kuogeshea mifugo.
Naye, Mwenyekiti wa Kijiji cha Chingurubila Bw. Bonifasi Manyonyi alisema, katika Kijiji hiki kina jumla ya kaya 101 na wafugaji 147 ambao tunategemea watanufaika na Josho hili pamoja na vijiji Jirani.
Katika ziara hiyo, wananchi wa Kijiji cha Chingurubila waliishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuwapatia fedha hizo kwa ajili ya ujenzi wa Josho, pia waliipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kwa kuwawezesha katika Ujenzi na kuhakikisha Josho linakamilika kwa wakati.
Pia Kamati ilitembelea na kukagua Kiwanja kilichotolewa na Wanakijiji cha Mariwanda, Kata ya Hunyari kwa ajili ya Ujenzi wa shule ya Awali na msingi.
Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji cha Mariwanda Bw. Jumanne Mwaibiro alisema, Kijiji hiki kina jumla ya vitongoji 16 na vitongoji vitatu vinapakana na Hifadhi ya Serengeti hivyo, aliiomba Kamati pamoja na Halmashauri kuwasaidia kujenga shule katika Kijiji chao kutokana na hatari ya kushambuliwa na Wanyama wakali.
Bw. Mwaibiro alisema, Kijiji hadi sasa kimeshatenga hekari 10 kwa ajili ya Ujenzi wa shule, ambapo hekari 5 tayari zimeshapimwa na hekari 5 bado hazijapimwa hivyo waliiomba Kamati kuwasaidia kupima hizo hekari 5 zilizobaki na kuwasaidia kupata hati miliki ya eneo.
“Wananchi wapo tayari kushirikiana na Halmashauri katika Ujenzi huo na kwa kuanza wameanza na usafishaji wa kiwanja.” Alisema Bw. Mwaibiro.
Kamati ilimshauri Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji kuitisha mkutano wa hadhara na Wanakijiji kwa ajili ya kujadiliana namna gani watashirikiana na Halmashauri katika Ujenzi wa shule hiyo kwa kubainisha mahitaji na changamoto walizonazo ikiwemo ya kupata wataalamu wa kupima Ardhi ili wawasaidie kupima hizo hekari 5 ambazo hazijapimwa na kuomba Wataalamu wa Ujenzi kuwapatia ramani sahihi katika ujenzi wa madarasa hayo.
“Wekeni juhudi sana katika suala hili la ujenzi wa shule kwa kuwataka kuwa na ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha ujenzi huo unatekelezwa na kukamilika kwa wakati ili hadi mwakani waweze kupokea wanafunzi wa Awali na msingi kwaajili ya kuanza shule”. Ilisema Kamati.
Naye, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Bw. Oscar Jeremiah Nchemwa alimwambia Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji baada ya mkutano huo ahakikishe anamuandikia Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri muhtasari ambao utaelezea mahitaji na changamoto wanazokabiliana nazo na namna gani washirikiana na Halmashauri katika Ujenzi huo.
Kibara Stoo.
Anuani ya Posta: 126, Bunda
Simu: 0282621055
Hamishika: 0742163056
Barua Pepe: ded@bundadc.go.tz
Haki Miliki@ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda