Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. George Simbachawene leo tarehe 19/6/2017 amebatilisha Maeneo ya Kiutawala ya Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na Halmashauri ya Mji wa Bunda. Mhe. Simbachawene alifikia maamuzi hayo baada ya kusikiliza kwa maakini michango ya washiriki mbalimbali wa kikao cha majumuisho kilichofanyika na kuona kuwa zoezi la mgawanyo liligubikwa na mgogoro uliosababishwa na mipaka iliyowekwa hapo awali kwa kuwa haikuzingatia lengo kuu la uanzishwaji wa Halmashauri hizo la kusogeza huduma karibu na Wananchi.
Akitoa ufafanuzi wa uamuzi huo, Mhe. Simbachawene alisema kuwa haiwezekani mamlaka moja iwe na eneo la kiutawala ambalo mwannchi wake akitaka huduma analazimika kuruka mamlaka nyingine. Alisema hivyo akitolea mfano eneo linalosimamiwa na halmashauri ya wilaya ya Bunda ambayo inaundwa na Tarafa 3 za Kenkombyo, Nansimo na Chamriho ambapo ili mwananchi toka tarafa ya Chamriho apate huduma toka makao makuu ya halmashauri yake itabidi azipite kwanza ofisi za halmashauri ya Mji na ndipo afike ofisi za halmashauri ya Wilaya.
Waziri Simbachawene alihitimisha uamuzi huo kwa kuitaka halmashauri ya Wilaya ya Bunda kukabidhi majengo yake yote kwa Halmashauri ya Mji na kwenda kujenga ofisi zake katika Jimbo la Mwibara lenye tarafa 2 za Nansimo na Kenkombyo. Wakati huo huo Mhe. Simbachawene ameagiza wasaidizi wake kuangalia namna ya kuunganisha Tarafa ya Chamriho na ile ya Serengeti yalipo Makao Makuu ya Halmashauri ya Mji kwa sasa ikiwa ni moja ya hatua za kuweka uwiano wa maeneo ya kiutawala na hivyo kurahisisha utoaji huduma kwa wananchi.
Kibara Stoo.
Anuani ya Posta: 126, Bunda
Simu: 0282621055
Hamishika: 0742163056
Barua Pepe: ded@bundadc.go.tz
Haki Miliki@ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda