Halmashauri ya Wilaya ya Bunda imejiwekea mkakati wa kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote wanaovamia maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya masoko. Mkakati huo umeelezwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Mhe. Isack Kabugu Maela wakati wa ziara ya uzinduzi wa masoko 6 yaliyojengwa na Serikali na kukaa kwa muda mrefu bila kutumika kutokana na sababu anuai ikiwemo baadhi ya maeneo ya masoko hayo kuvamiwa na wananchi. “Ninaziagiza Serilkali za vijiji vyote vyenye masoko kuhakikisha zinatoa taarifa mara moja kuhusu wananchi waliovamia maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya masoko hayo ili hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao”
Ziara hiyo ya uzinduzi wa masoko hayo ilifanyika kuanzia tarehe 10/7/2018 hadi tarehe13/7/2018 katika masoko yaliyopo katika vijiji vya Masahunga, Nansimo, Kibara, Nakatuba, Iramba, Hunyari na Mihingo. Uzinduzi wa masoko hayo unalenga katika kuborosha upatikanaji wa bidhaa mbalimbali kwa wakazi wanaozunguka masoko hayo na kuboresha kipato kwa wakulima wa mazao ambao wamekuwa wakiuza mazao yao kwa bei ndogo sana kwa madalali ambao wamekuwa wakijipatia faida kubwa. Pia uzinduzi huo unalenga katika kuongeza vyanzo vya mapato ya Halmashauri kupitia ushuru na tozo zitakazokuwa zikitozwa katika masoko hayo.
Akizungumza na wakazi wa kijiji cha Masahunga wakati wa uzinduzi wa soko hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Bwana Amosy Kusaja aliwahimiza wananchi kutumia fursa hiyo vizuri katika kujiongezea kipato kwa kuhakikisha kuwa wanatuma maombi mara moja ya kupewa maeneo ya biashara katika soko hilo. “Ni jukumu lenu kuhakikisha mnatumia soko hili katika kujiongezea kipato kupitia shughuli mbalimbali za ujasiliamali” Katika kuhamasisha wananchi kutumia masoko hayo, Mkurugenzi huyo alitoa “offer” kwa wafanyabiashara wote wa maeneo hayo kuanza kuuza bidhaa zao katika masoko hayo mara moja bila kutozwa tozo au ushuru wowote ule kwa kipindi cha siku hamsini kuanzia tarehe 10/7/2018, baada ya hapo ndipo ushuru na tozo mbalimbali zitaanza kukusanywa na Halmashauri.
Katika uzinduzi huo wa masoko 7, Afisa Masoko wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Bwana Mtaki Zacharia alitumia fursa hiyo kutoa ufafanuzi wa taratibu za upataji wa maeneo ya kufanyia biashara katika masoko hayo na tozo zitakazolipwa na wafanyabiashara katika masoko hayo. Bwana Mtaki alieleza kuwa Kwa yeyote anayehitaji eneo la biashara anapaswa kuandika barua ya maombi kwenye uongozi wa Serikali ya kijiji. Baada ya maombi hayo kukubaliwa mwombaji ataingia mkataba wa kisheria na Halmasahuri ya Wilaya na kisha atapaswa kulipia kiasi cha shilingi 5,000/= kwa kila mwezi kulingana na idadi ya miezi anayohitaji. Baadaya hapo Kamati ya soko itakuwa inakusanya ushuru wa shilingi 200/= kila siku. Ushuru huu ni kwa wale watakaopata meza zilizo ndani ya masoko hayo. Aidha, kwa waombaji watakaokoswa meza ndani ya masoko hayo watatengewa maeneo nje ya majengo ya masoko hayo, watapewa ramani ya vibanda ambavyo watajenga kwa gharama zao na kisha kutumia vibanda hivyo bila malipo ya kila mwezi mpaka hapo gharama walizotumia kujenga vibanda hivyo zitakapokuwa zimekwisha, isipokuwa watakuwa wakilipa ushuru wa shilingi 100/= kila siku. Afisa masoko huyo alihitimisha kwa kusema kuwa mfanya biashara yeyote atakayekuwa anafanya biashara yake eneo tofauti na masoko hayo atatozwa faini ya shilingi 50,000/= bila kujali ukubwa wa biashahra yake.
Nae mwakilishi wa Afisa Kilimo wa Halmashauri Bwana Zabroni Mashauri. alitumia fursa hiyo kutoa maelekezo kwa wananchi wote kuhakikisha kuwa kuanzia sasa mazao yote ya kilimo na mifugo yanaouzwa katika maeneo ya masoko hayo na si vinginevyo. Bwanan Zabroni alizitaka Serikali za vijiji kuhakikisha zinaunda sheria ndogondogo za kuwadhibiti wakulima na wafanyabiashara wanaouza na kununua mazao na mifugo maeneo tofauti na masoko hayo. Pia aliwataka wananchi kuhakikisha matumizi sahihi ya vipimo yanazingatiwa kwa kuhakikisha kuwa mizani yote inayotumika iwe imehakikiwa na wakala wa vipimo wa Serikali ili kuwaepusha wakulima kupunjwa na wanunuzi wa mazao yao.
Kibara Stoo.
Anuani ya Posta: 126, Bunda
Simu: 0282621055
Hamishika: 0742163056
Barua Pepe: ded@bundadc.go.tz
Haki Miliki@ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda