Mkuu wa Wilaya ya Bunda Mhe. Mwl. Lydia Bupilipili amezindua zoezi la utoaji wa chanjo ya kujikinga na ugonjwa hatari wa Saratani ya mlango wa kizazi. Uzinduzi huo umefanyika siku ya tarehe 23/4/2018 katika Kata ya Nyamuswa ukiongozwa na kauli mbiu isemayo “Jamii iliyopata chanjo ni jamii yenye Afya. Timiza wajibu wako”
Akitoa hotuba ya uzinduzi Mkuu huyo wa Wilaya aliwataka wananchi kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika zoezi hilo ili liwe na ufanisi kama lilivyokusudiwa ili kuiepusha jamii ya wana Bunda na ugonjwa hatari wa Saratani ya mlango wa kizazi kwa wanawake.
Aidha, aliwaonya wananchi kuhakikisha wanaepuka imani potofu zinazowaaminisha kuwa chanjo hiyo ina madhara kwa walengwa wa zoezi hilo. Mkuu huyo wa Wilaya aliwaonya wananchi wote wanaoeneza uvumi kuwa chanjo hiyo itasababisha ugumba kuacha mara moja tabia hiyo ya uzushi. Aliwataka wananchi kutoa ushirikianao kwa kuwafichua wale wote wanaoeneza uvumi huo ili wachukuliwe hatua stahiki za kisheria. “Serikali imejipanga kuhakikisha zeoezi hili linafanyika kwa ufanisi mkubwa, na yeyote atakayethubutu kuvuruga zoezi hili atakiona cha mtema kuni”
Mkuu huyo wa Wilaya aliendelea kusisitiza kuwa mtaji mkubwa wa mwanadamu yoyote ni afya njema ambayo itamwezesha kutekeleza majukumu yake ya kila siku kwa ufanisi na kujiletea maendeleo bila kuathiri kipato chake kwa kugharamia matibabu makubwa ambayo angeweza kuyaepuka kwa njia ya chanjo mbalimbali zinazotolewa na Serikali tena kwa gharama kubwa.
Awali akiongea na wananchi, Diwani wa Kata ya Nyamuswa Mhe. Fyeka Sumera aliwasihi wananchi hao wa Kata ya Nyamuswa kuacha kushikilia imani potofu zinazowazuia kuwapeleka wagonjwa wao kupata huduma za kitabibu katika vituo vya afya na badala yake kuwapeleka kwa waganga wa kienyeji kwa imani kuwa wagonjwa hao wamerogwa.
Naye Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Dk. Nuru Yunge aliwaasa wananchi wote kuhakikisha kuwa wanashiriki kikamilifu katika mazoezi mbalimbali ya afya yanayofanyika ili kujikinga na maradhi mbalimbali yanayoweza kuepukwa kwa njia ya chanjo. Dk. Nuru Yunge pia alieleza kuwa sambamba na uanzishajwaji wa chanjo hiyo ya kuzuia Saratani ya mlango wa Kizazi, pia unafanyika uzinduzi wa chanjo ya Polio kwa njia ya sindano ambayo motto atapewa mara atakapofikisha umri wa wiki 14.
Akisoma taarifa ya Hamashauri mbele ya mgeni rasmi, Mratibu wa Chanjo wa Halmashauri Bi. Magreth Nyambwa alieleza kuwa halmashauri imejipanga kutoa chanjo ya kujikinga na Saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana wapatao 3932 ili kuwaepusha na athari za ugonjwa huo hatari na kuwa na jamii yenye afya itakayowawezesha kutekeleza majukumu yao ya uzalishaji mali ili kujiletea maendeleo
Kibara Stoo.
Anuani ya Posta: 126, Bunda
Simu: 0282621055
Hamishika: 0742163056
Barua Pepe: ded@bundadc.go.tz
Haki Miliki@ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda