Wakulima na Wadau wengine wa kilimo Bunda wapata mafunzo ya kimkakati kuzuia upotevu wa Mazao
Na Nuru Ally, Bunda DC
KATIKA kuhakikisha wakulima wilayani Bunda,Mkoa wa Mara wanajengewa uwezo ili kuimarisha kilimo ikiwa ni pamoja kushiriki katika kilimo cha kisasa,kuongeza uwezo wa uzalishaji,Wizara ya kilimo imeendesha mafunzo maalumu iliyowahusisha wadau mbalimbali wakilimo.
Akizungumza katika mafunzo hayo yaliyofanyika jana katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Kibara, Bunda Afisa Kilimo Mkuu Bi. Margaret Natai kutoka wizara hiyo,alisema yameandaliwa maalum kwa ajili ya mkakati maalum wa kupunguza upotevu wa mazao baada ya kuvuna.
“Upotevu wa Mazao ni mkubwa, sisi wizara hatuwezi kuendelea kutazama hali hiyo ikiendelea” alisema.
Aidha,Margaret alitaja vyanzo mbalimbali vinavyosababisha upotevu wa mazao baada ya mavuno ni pamoja na teknolojia duni za kuhifadhi mazao,ufahamu mdogo wa wadau na miundombinu duni ya usafirishaji.
Pia,alisema changamoto hiyo inatokana na ukosefu wa masoko ya uhakika,kutokuwepo kwa mitaji,uwekezaji hafifu katika tafiti na ubunifu na teknolojia duni katika uvunaji na ukaushaji.
“Wizara imeandaa mafunzo haya ikiamini kuwa mtafahamu namna ya kudhibiti mazao ili yasipotee,’’ alisema Afisa Kilimo huyo akiongea na Wakulima na Wadau wengine wa kilimo waliohudhuria mafunzo hayo.
Awali akizungumza katika mafunzo hayo,Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Steven Ochieng aliwapongeza waliofanikisha kuandaliwa kwake akiamini yatakuwa msaada kwa maendeleo ya kilimo wilaya ya Bunda.
‘’Wizara ya kilimo imeleta mafunzo haya wakati mwafaka wa mavuno,’’alisema Kaimu Mkurugenzi Mtendaji.
Bw. Ochieng alisema kuwa mafunzo hayo yatasaidia kulinda maendeleo ya uchumi pamoja na kusaidia wakulima kuzalisha kulingana na mahitaji.
Kwa upande wa mdau wa kilimo, Michael Kweka alisema mafunzo hayo yatasaidia kukabiliana na upotevu wa mazao na kuahidi kuwa baada ya kupokea elimu hiyo atakuwa mwalimu na mjumbe kwa Wakulima wengine juu ya utunzaji,uvunaji na usindikaji ili kuhakikisha yanawafikia walaji kwa wingi
Kupitia mafuzo haya wakulima pamoja na wadau wengine walielimishwa juu ya athari za upotevu wa mazao baada ya kuvunwa ikiwemo kutetereka kwa lishe na afya ya jamii huku pia ikisababisha athari za kiuchumi.
Kabla ya mafunzo hayo baadhi ya washiriki hawakuwa na uelewa kuhusu namna mazao yanavyoweza kupotea baada ya mavuno,lakini baada ya elimu hiyo wengi walionesha kutambua namna mazao yanavyoeza kupotea na jinsi ya kupunguza upotevu huo.
Aidha, kupitia mkusanyiko huo wadau na wakulima kwa ujumla waliweza kuunda jukwaa la utekelezaji ambalo litasaidia kupata ushauri na ushawishi mbalimbali ili kuhakikisha mkakati huo unatekelezeka.
Inakadiriwa kuwa kiasi cha asilimia30 hadi 40 ya mazao yanayozalishwa nchini kila mwaka hupotea kabla yakuwafikia walaji kutokana na sababu mbalimbali mojawapo ikiwa ni utunzaji duni.
Ili kudhibiti hali hiyo,Serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya kilimo imeamua kuandaa Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Mazao baada ya kuvuna.
Kibara Stoo.
Anuani ya Posta: 126, Bunda
Simu: 0282621055
Hamishika: 0742163056
Barua Pepe: ded@bundadc.go.tz
Haki Miliki@ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda