Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Bunda, Bi. Changwa M. Mkwazu akimkaribisha mgeni rasmi ambaye ni mkuu wa wilaya ya Bunda Mh. Dr. Vicent Anney katika kikao kazi cha Watendaji wa kata, vijiji na maafisa ugani kilichofanyika katika ukumbi wa kanisa Katoliki lililopo Kibara siku ya tarehe 25/9/2023.
Bi Mkwanzu alisema, lengo la kikao hiki ni kuwajengea uelewa katika utendaji wao wa kazi huko katika kata na vijiji vyao, mbali na kikao hiki Watendaji wa kata, na vijiji watapatiwa mafunzo ya matumizi ya mfumo wa FFARS.
‘Mheshimiwa mgeni rasmi, kupitia kikao kazi hiki tutawajengea uwezo wa kusimamia miradi vizuri katika kata na vijiji, usimamizi wa mapato katika halmashauri yetu na usimamizi mzuri wa ustawi wa Afya katika kata na vijiji vyao’. Alisema bi. Mkwazu.
Naye, Mkuu wa wilaya ya Bunda Mh. Dr. Vicent Anney, alimshukuru Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Bunda kwa kumkaribisha kufungua kikao kazi cha Watendaji wa kata, Vijiji na Maafisa ugani.
Mh. Dr. Anney alisema, siku ya leo nina mambo kadhaa ya kuwaambia watumishi wote mliopo hapa kwa kuanza, aliwaambia watumishi wote katika halmashauri wanapaswa kuheshimu muda wa kazi, na sio kwa Watendaji kata, vijiji na Maafisa ugani tu, suala la muda kazini ni la kila mtumishi wa umma aliyepo mahali hapa na kuhakikisha kila mtu anakuwepo katika eneo lake la kazi kwa wakati sahihi na kufanya majukumu yake.
Pia aliongelea suala la ukusanyaji mapato katika halmashauri, kwa kuwasisitiza Watendaji kata, vijiji na Maafisa ugani wote kushirikiana katika ukusanyaji wa mapato ya halmashauri kwa usahihi.
‘Niwaombe tusaidiane katika ukusanyaji wa mapato, msiseme ni kazi ya halmashauri peke yake wote mnawajibu wa kukusanya mapato kwa usahihi mnatakiwa mshirikiane wote watendaji kata, vijiji na Maafisa ugani.’’ Alisema Mkuu wa wilaya.
Mh. Dr. Anney alisema kila mmoja kwenye kata na vijiji huko ahakikishe mapato yote yanakusanywa kwa asilimia 100, hivyo alimuagiza Mkurugenzi Mtendaji kuhakikisha baada ya kumalizika mafunzo haya kila Mtendaji wa kata na kijiji kuhakikisha anapatiwa POS kwa ajili ya kwenda kukusanya mapato.
Mkuu wa wilaya aliongelea suala la usimamizi wa miradi kwa Watendaji wa kata na vijiji, kwa kuhakikisha wanaisimamia miradi yote iliyopo katika kata na vijiji vyao kwa kuhakikisha inasimamiwa kwa usahihi na kwa viwango sahihi kabisa.
‘ Nimechoka kubaini miradi mibovu kila mara, sababu huko chini kuna watendaji kata, vijiji hadi tarafa ambao wanapaswa kuisimamia miradi hii vizuri na kuhakikisha inakuwa na viwango sahihi, sisi sote ni watendaji wa serikali tunatakiwa tukafanye kazi kwa bidii’. Alisema.
Pia, aliwaambia Maafisa ugani hasa Maafisa kilimo kuhakikisha wanasimamia vizuri kilimo chetu katika kata na vijiji huko ili kuhakikisha halmashauri haipotezi mapato yake.
Mkuu wa wilaya amewataka Maafisa ugani kushirikiana na watendaji kata na vijiji kuhakikisha wanapata takwimu sahihi kabisa kwa upande wa kilimo na mifugo ambazo zitaisaidia halmashauri kukusanya mapato yake kwa usahihi, na pia itasaidia kuonyesha muelekeo wa halmashauri ulipo katika sekta ya kilimo na mifugo.
Mh. Dr. Anney aliwataka kila Afisa kilimo katika kata na kijiji ahakikishe anaanzisha shamba darasa katika kata na kijiji alichopo, shamba darasa hilo ni kwa mazao ya mahindi, viazi, pamba, dengu na mtama.
Mafunzo haya ya matumizi ya mfumo wa FFARS unaratibiwa na idara ya mipango na fedha ambao ulihudhuriwa na Watendaji kata 19, Watendaji wa vijiji 78 na Maafisa Ugani 20 kutoka halmashauri ya wilaya ya Bunda.
Kibara Stoo.
Anuani ya Posta: 126, Bunda
Simu: 0282621055
Hamishika: 0742163056
Barua Pepe: ded@bundadc.go.tz
Haki Miliki@ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda