Watu wenye Ulemavu katika kata ya Hunyari,Mugeta na kata Mihingo wamehimizwa kuachana na mila potofu ya unyanyasaji wa kijinsia ikiwemo ukeketaji kwa wanawake,kuwafungia watu wenye ulemavu majumbani na kutokuwepo kwa usawa kati ya wanaume na wanawake.
Hayo yameelezwa na Afisa Ustawi wa jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ambaye pia ni Mratibu wa watu wenye Ulemavu Bi.Maria John alipokuwa akiendelea na ziara yake siku ya tarehe 8/11/2024, ya kuwatembelea watu wenye ulemavu ndani ya Halmashauri hiyo, huku lengo kuu likiwa ni kutoa Elimu ya ukatili wa kijinsia kwa watu walemavu, Uundaji wa vikundi vya mikopo kwa watu wenye ulemavu na kushiriki katika uchaguzi wa vyama vya walemavu na serikali za mitaa.
Amesema kuwa elimu ya unyanyasaji wa kijinsia imekuwa ikitolewa kwa wingi lakini bado kuna baadhi ya watu wamekuwa wakitumia mila potofu kuendeleza ukatili katika jamii zao, sambamba na hayo amewahimiza watu wenye ulemavu kuunda vikundi ili waweze kuchukua mikopo inayotolewa na halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
"Niwaombe tujitokeze kupaza sauti pindi tunapoona wenzetu wanafanyiwa ukatili ili tuweze kusaidiana sisi kama sisi na ofisi za kutoa taarifa zipo nyingi sana kuanzia wahudumu ngazi ya Afya ambao wapo katika vitongoji vyetu lakini pia tupendane na tuache kufanyiana vitendo vya kikatili, niwakumbushe tu kuwa kuna ukatili wa aina nyingi sana kama ukatili wa kimwili, ukatili wa kisaikolojia, Ukatili wa kihisia na ukatili wa kiuchumi kwahiyo niwaombe tulindane sisi kwa sisi"Amesema Bi. Maria
Kwa upande wake Mratibu wa Uibuaji wa fursa na vikwazo kwa Maendeleo wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Ndugu Emson Noel amewataka watu wenye ulemavu kutojishusha thamani na kutochukulia ulemavu wao kama chanzo cha kushindwa kufanya maendeleo na amewahimiza kuchangamkia fursa ya mikopo inayotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ili iweze kuwasaidia kukua kiuchumi.
"Kuwa na ulemavu wa viungo siyo ulemavu wa akili na tusishinde kufanya maendeleo kisa ulemavu wetu, na waombeni sana mjitokeze kwa wingi kuchukua mikopo ambayo itasaidia kutengeneza kipato chetu wenyewe na kupunguza kuwa tegemezi katika familia zetu"Amesema Noel
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Watu wenye Ulemavu Tanzania katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Ndugu Sabasaba Mseveni Haji amewahimiza wanachama wote kujitokeza kushiriki uchaguzi unaotarajia kufanyika tarehe 15/11/2024 na kusema kuwa mara ya mwisho uchaguzi huo ulifanyika mawaka 2019 na kuwataka wanachama kutumia nafasi hii kugombea na kuchagua viongozi sahihi kwa upande wao.
Hata hivyo watu wenye ulemavu katika kata hizo wamesema changamoto kubwa ya wao kushindwa kujitokeza kuomba mikopo hiyo ni ukosefu wa elimu sahihi ya uombaji wa mikopo na changamoto ya kuandaa andiko la vikundi huku wakimshukuru Afisa ustawi wa jamiikwa kutoa Elimu hiyo na kuhaidi kujitokeza kuomba mikopo katika robo ya pili ya utoaji wa mikopo.
Kibara Stoo.
Anuani ya Posta: 126, Bunda
Simu: 0282621055
Hamishika: 0742163056
Barua Pepe: ded@bundadc.go.tz
Haki Miliki@ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda