Mafunzo ya kuwajengea uelewa Watalaamu wa sekta mbalimbali namna ya kuandaa Mipango, Bajeti, Usimamizi wa Fedha na Utoaji wa Taarifa kupitia mifumo ya PLANREP na FFARS katika halmashauri ya Wilaya ya Bunda yameanza leo katika ukumbi wa halmashauri ambapo takribani washiriki 40 walihudhuria mafunzo hayo. Mafunzo haya yamelenga kutambulisha mfumo ulioboreshwa wa mipango na bajeti wa PLANREP na mfumo mpya wa FFARS ambao utatumika kusimamia matumizi ya fedha na utoaji wa taarifa katika vituo vya kutolea huduma katika sekta za Afya na Elimu.
Akizindua mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kupitia kwa Mwakilishi wake alisisitiza umuhimu wa mafunzo hayo kwa Washiriki ambao pia ni Wakuu wa Idara na Wasaidizi wao kuzingatia mafunzo hayo yatakayofanyika kwa siku 5 ili kupata uelewa unaotakiwa na hivyo kuwa na uwezo wa kutumia mifumo hiyo kwa ufanisi. Mafunzo hayo ni muendelezo wa mafunzo ya aina hiyo yaliyofanyika Mkoani Mwanza na yanafadhiliwa na mradi wa PS3 kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI).
Wakati mafunzo hayo yakiendelea, timu ya Wawezeshaji ngazi ya Taifa na Mkoa wa Mara ilifika kuona namna mafunzo yalivyokuwa yakifanyika na kuwapongeza Wawezeshaji pamoja na Washiriki kwa namna walivyojipanga kufanikisha zoezi hilo. Pamoja na mambo mengine, timu hiyo ilitatua na kutoa ufafanuzi kwa baadhi ya changamoto zilizotolewa kwao na washiriki wa mafunzo hayo.
Kibara Stoo.
Anuani ya Posta: 126, Bunda
Simu: 0282621055
Hamishika: 0742163056
Barua Pepe: ded@bundadc.go.tz
Haki Miliki@ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda