Maaadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yamefanyika Wilayani Bunda katika Viwanja vya Shule ya Msingi Kambubu, Kijiji cha Kambubu, Kata ya Nyamang'uta, Tarafa ya Chamriho. Maadhimisho hayo yaliyobeba ujumbe mahsusi wa "MAENDELEO ENDELEVU 2030: IMARISHA ULINZI NA FURSA SAWA KWA WATOTO" yalinuia kuikumbusha jamii katika kutekeleza wajibu wake wa kumthamini na kumhudumia mtoto wa Kiafrika ili apate fursa ya kujengewa uwezo kwa ajili ya maisha yake ya baadaye kama walivyo watoto wengine Duniani.
Katika maadhimisho hayo ambayo yaliandaliwa na Shirika la PCI la Marekani kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, mgeni rasmi alitakiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara ila kwa kuwa alibanwa na majukumu mengine, aliwakilishwa na Mkuu Wilaya ya Bunda Ndg. Lidya Bupilipili. Pamoja na mambo mengine, mkuu huyo wa Wilaya alisisitiza juu ya Viongozi na Watendaji ngazi ya Halmashauri, Kata, Vijiji, Shule, Wazazi na Jamii kwa ujumla kuelewa kuwa jukumu la kulea na kuwajengea mazingira mazuri Watoto ni lao na si la Wafadhili na akaendelea kusema kuwa anawashukuru sana watu wa PCI kwa kuiamsha jamii hiyo ili ijitambue na kuchukua hatua. Hivyo akatoa agizo kwa kwa jamii husika kuhakikisha kuwa mila na desturi zinazowanyima watoto fursa ya kujenga maisha yao ya baadaye kama vile kuoza watoto wa kike katika umri mdogo kwa sababu ya kupata mali na kuwakosesha elimu ambayo ndio nguzo kuu ya maendeleo yao kukoma mara moja.
Pia, katika maadhimisho hayo, mgeni rasmi aliweza kuzindua huduma mbalimbali shuleni hapo ambazo zimefadhiliwa na Shirika la PCI kama vile Vyoo Bora, Bustani ya mbogamboga kwa ajili ya kuwawezesha wanafunzi kupata chakula shuleni, Chumba cha darasa la awali kikiwa kimesheheni vifaa mbalimbali vya kujifunzia, Miradi ya kijasiriamali kwa kinamama, nk.
Kibara Stoo.
Anuani ya Posta: 126, Bunda
Simu: 0282621055
Hamishika: 0742163056
Barua Pepe: ded@bundadc.go.tz
Haki Miliki@ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda