Halmashauri ya wilaya ya Bunda Siku ya tarehe 26/9/2023 iliadhimisha wiki ya Afya na Lishe kwa kuwashirikisha wadau na wataalamu wa afya kushiriki maadhimisho hayo ambayo yalifanyika katika shule ya awali iliyopo kata ya Kibara.
Kaimu mwenyekiti wa kamati ya maendeleo katika kata ya Kibara, Bw. Mtaki Didas Nagabona alisema hii ni wiki ya maadhimisho ya Afya na Lishe ambayo huadhimishwa kila baada ya miezi mitatu kwa mwaka.
Bw. Nagabona alisema Afya na Lishe inaanzia kwa watoto wenye umri kuanzia miaka sifuri (0) na kuendelea hivyo alisisitiza watu wote katika jamii kuzingatia Lishe iliyo bora kuanzia elimu ya awali hadi ya sekondari watoto wetu wanapaswa kuwa na Afya bora na kuzingatia Lishe iliyo sahihi.
Akiongea na wanaume wa kata ya Kibara, Kaimu mwenyekiti wa kamati ya maendeleo alisema, suala la Afya na Lishe bora ni kwa watu wote na sio kuwaachia wanawake tu huko katika familia zenu, tukiwa kama wanaume katika kata hii tunapaswa tuzingatie ustawi wa Afya zetu na familia zetu kwa ujumla kwa kuhakikisha tunafuata muongozo wa kula Lishe iliyo bora.
“Serikali kupitia mpango wa TASAF kunusuru kaya maskini imewawezesha watu wengi katika masuala ya Afya na Lishe bora kwa kuhakikisha kila kaya inakuwa na Afya njema kwa kupata Lishe iliyo bora.”
Naye, Afisa Mtendaji wa kata ya Kibara, Bi. Beatrice Lawrance Batunika alisema, katika kuhakikisha wiki ya Afya na Lishe kwenye kata unafanikiwa alihakikisha wanashirikiana na watendaji wa vijiji, Mheshimiwa diwani pamoja na wadau mbalimbali katika kuhakikisha wanafuata muongozo wa Afya na Lishe kuanzia shule za awali hadi sekondari.
“Tumekuwa tukitoa elimu kwa jamii kwa njia ya nadharia, kwa kwenda kwenye shule za awali hadi sekondari kuwaelekeza namna gani ya kuandaa Lishe iliyo bora kwa watoto kwa kuzingatia muongozo kutoka kwa wataalamu wa Lishe. Pia tunawafundisha kwa vitendo kwa kuandaa makundi yote muhimu ya vyakula kama tunavoelekezwa na wataalamu wa Lishe bora.” Alisema Bi. Batunika.
Naye, Afisa Lishe wa mkoa wa Mara Bw. Benson Sanga aliwasisitiza wananchi wa kata ya Kibara kuhakikisha wanafuata maelekezo sahihi kutoka kwa wataalamu wa Afya na Lishe katika kuhakikisha wanakula vyakula vilivyo katika makundi muhimu kama yanavoelekezwa na wataalamu wa Afya na Lishe.
“Katika suala hili la Afya na Lishe, walengwa haswa ni wazee, wajawazito na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano. Hivyo aliwasisitiza kuhakikisha makundi haya yanapatiwa Lishe iliyo bora kwa kufuata muongozo kutoka kwa wataalamu wa Afya.” Alisema Bw. Sanga.
Naye, muhudumu wa Afya katika kata ya Kibara Bw. Dismas Pastory alisema, tupo vizuri pamoja na changamoto ndogondogo zilizopo, katika kata yetu ni mara chache sana tunaweza kupata watoto wenye changamoto zinazotokana na Lishe.
Kibara Stoo.
Anuani ya Posta: 126, Bunda
Simu: 0282621055
Hamishika: 0742163056
Barua Pepe: ded@bundadc.go.tz
Haki Miliki@ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda