Mkuu wa Wilaya ya Bunda Mh. Dr. Vicent Anney siku ya tarehe 10/10/2023 katika kijiji cha Mariwanda, Kata ya Hunyari alizindua kikundi cha Vijana Moto kinacho jishughulisha na uzalishaji Unga wa Lishe.
Mh. Dr. Anney aliweza kutembelea na kujionea shughuli za Kikundi wanazofanya, ikiwemo mashine ya kusaga na kukoboa unga pamoja na kujionea upakiaji wa unga katika vifungashio vyake na mashine wanayotumia katika ufungaji.
Mkuu wa Wilaya aliwapongeza Vijana kwa kuanzisha kiwanda katika kijiji chao kwani kitawarahisishia Wananchi hasa wanaoishi katika kijiji hiki na vijiji jirani pamoja na Halmashauri kwa ujumla kwa kuweza kupata unga ulioongezwa virutubisho, hivyo aliwataka Wananchi kuwaunga mkono Vijana hao kwa kuhakikisha wanaenda kusaga katika mashine hiyo na kununua bidhaa kutoka katika kikundi hicho.
“Niwapongeze Vijana kwa kuwa na ubunifu hata wa kuwa na vifungashio vinavoweza kuwatambulisha kiurahisi, hivo mnatakiwa muanze na kusambaza bidhaa hizi katika maeneo mbalimbali hadi Mjini msiishie hapa tu, pia muanze kujitangaza kupitia mitandao ya kijamii na kwenye redio mbalimbali ili muweze kujulikana zaidi.” Alisema Mkuu wa Wilaya.
Pia alimshukuru Mh. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kulifanya suala hili la Lishe kuwa muhimu katika jamii yetu, kwa kuona Watanzania wanatakiwa kupata virutubisho vya kutosha.
“Chakula kilicho na virutubisho ni dawa, niwaombe Wajumbe, Waheshimiwa Madiwani, Viongozi wote wa vijiji na Kata kuwahamasisha Wananchi kuja kusaga hapa kwa ajili ya kupata virutubisho vinavyotakiwa katika miili yao, aliwaagiza kuendelea kutoa elimu kwa Wananchi kula vyakula vyenye virutubisho wanapoa andaa Lishe. Ajenda hii ya Lishe ni ya Mkoa mzima, ndio maana Mh. Rais anasisitiza watu wote kupata vyakula vyenye virutubisho vya kutosha hasa kwa watoto shuleni kwa kuhakikisha wanapatiwa vyakula vyenye virutubisho vya kutosha na sahihi katika Lishe.” Alisema Dr. Anney.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Bi. Changwa M. Mkwazu alimwambia Mkuu wa Wilaya tunashukuru kwa kupata kiwanda hiki katika Halmashauri yetu, kwani huwa tunapimwa kwa vigezo mbalimbali, mojawapo ni kuhakikisha watoto wetu shuleni wanapewa vyakula vyenye virutubisho vya kutosha katika uandaaji wa Lishe.
“Ombi langu Mh. Mkuu wa Wilaya ninaomba uendelee kuhamasisha huko katika maeneo mengine unapokuwa unatembelea ili waweze kuja kuwaunga Vijana hawa kwa kuhakikisha wananunua bidhaa zao na kuja kusaga katika mashine hii, tunakushukuru kwa kuja kututembelea na kuzindua kikundi hiki. Alisema Bi. Mkwazu.
Mwenyekiti wa Kikundi cha Vijana Moto Bw. Wasembe Lusinde alisema Kikundi hiki kilianzishwa mnamo tarehe 10/5/2019 ambapo kilipata hamasa kubwa kutoka ofisi ya Maendeleo ya Jamii ya Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
Alisema katika mradi huu wa uzalishaji wa Unga wa Lishe hadi sasa wamezalisha kilo 1605 ambayo ni sawa na mifuko 321 yenye ujazo wa kilo 5 kila mfuko. Kilo 1355 ambazo ni sawa na mifuko 271 tayari zimeshauzwa, kilo 250 ambazo ni sawa na mifuko 50 zipo stoo bado hazijauzwa.
Pia tunavyo vifungashio 1800 ambavyo viko wazi hadi sasa vyenye thamani ya Shilingi 1,000,000/- Aidha tuna mahindi magunia mawili yenye thamani ya Tshs 240,000/- ambayo bado hayajatumika.
Bw. Lusinde alisema, Unga wa Lishe upo wa aina mbili na unapakiwa kwa kilo 5 kila mfuko wa unga wa Dona unauzwa Ths 10,000/- na Unga wa Lishe wa Sembe unauzwa Tshs 12,000/-.
Kikundi hiki kinafadhiliwa na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii kwa kupewa mkopo wa 10% ya mapato ya ndani kwa ajili ya kuwawezesha Wanawake, Vijana na watu wenye Ulemavu.
Kibara Stoo.
Anuani ya Posta: 126, Bunda
Simu: 0282621055
Hamishika: 0742163056
Barua Pepe: ded@bundadc.go.tz
Haki Miliki@ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda