Diwani wa Kata ya Iramba, ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Mh. Charles Manumbu siku ya tarehe 17/1/2024 amefanya kikao na Wananchi wa Kata ya Iramba, iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
Mkutano huo ulifanyika katika shule ya Sekondari Kwiramba baina ya Wazazi/Walezi, Kamati ya shule pamoja na Wanafunzi, lengo likiwa ni kuangalia na kutathimini maendeleo ya Elimu katika Kata hiyo.
Mh. Manumbu alisema nimeona ni muhimu tukiwa ni Wazazi na Walezi wa Wanafunzi wetu tukutane, tujadiliane, tuelezane na tufanye maazimio ambayo ni lazima tuyazingatie na tuyatekeleze ili kuweza kuinua kiwango cha ufaulu kwa Wanafunzi katika Kata hii. Kufanya tathimini ya miaka mitatu kwa matokeo ya darasa la Nne, la Saba, kidato cha Pili na cha Nne.
Walimu wa shule za Msingi na Sekondari waliweza kuwasilisha taarifa zao za matokeo kwa madarasa hayo kwa kipindi cha miaka mitatu, kwa kueleza changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo Wanafunzi hao hadi kupelekea ufaulu mdogo katika Kata hiyo.
Wazazi/walezi, nao walipata wasaa wakuchangia katika mkutano huo, hivyo, walijadiliana kwa pamoja kuona ni namna gani wanaweza kuzitatua changamoto hizo zilizotajwa na Walimu hao ambazo ni umbali wa kutoka nyumbani hadi shuleni, uhaba wa Walimu katika shule ya Kwiramba, pamoja na utoro sugu.
Mwenyekiti wa bodi ya shule ya Kwiramba, Bwana Fiti Mjalifu aliwataka Wazazi na Walezi kujitathimini katika masuala ya Elimu kwa Watoto wao kwa kuhakikisha wanawahimiza kufika shuleni kwa wakati na kuhudhuria vipindi shuleni kwa kuhakikisha kila siku wanakagua madaftari yao, pia aliwataka kuwafundisha Watoto wao maadili yaliyo mema na sio kuwategemea Walimu peke yao kwenye suala na nidhamu.
“Wazazi na Walezi tukizingatia haya itasadia kupunguza utoro sugu kwa Wanafunzi na kuwafanya kuwa na maadili yaliyo mema, hivyo itachangia kuongeza kukuza ufaulu kwa Wanafunzi katika shule hii ya Sekondari.” Alisema Bw. Mjalifu.
Wazazi na Walezi waliomba Walimu wa masomo katika Sekondari ya Kwiramba waongezwe, pamoja na kujengewa mabweni kwa Watoto wa kike hasa wa kidato cha Pili na cha Nne.
Naye, Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Ndugu Wandere Lwakatare aliwaahidi Wazazi na Walezi kumleta Mhandisi wa Halmashauri kwa ajili ya kuja kuangalia na kushauri kuhusiana na baadhi ya majengo yaliyopo shuleni hapo kama yatatafaa kukarabatiwa kwa matumizi ya mabweni ya Wasichana hasa kwa kidato cha Pili na cha Nne.
Ndugu Lwakatare, aliwasisitiza Walimu kupenda kutumia lugha ya Kiingereza mara kwa mara ili Wanafunzi waweze kuijua na kuizoea kuitumia ambapo itawasaidia katika kuelewa masomo yao na kuwasaidia kufanya vizuri katika mitihani hayo, sababu masomo yote yanafundishwa kwa lugha ya Kiingereza.
Suala la kuongezewa Walimu katika shule hiyo, Ndugu Lwakatare aliwaahidi kulichukua na kulifikisha sehemu husika ambao ndio wanaowapangia Walimu vituo vya kazi.
Katika mkutano huo viongozi wa Serikali, Wazazi na Walezi waliazimia mambo yafuatayo, ambayo ni Wazazi na Walezi kuhakikisha wanakuja shuleni mara kwa mara kwa ajili ya kufuatilia maendeleo ya Watoto wao na kuhakikisha wanawahimiza kudhuria vipindi vyote shule kwa kuhakikisha wanakagua madaftari yao kila siku, kuhakikisha wanachangia Lishe shuleni, ili Watoto waweze kula chakula shuleni.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Wananchi kutoka vijiji vitano vilivyopo katika Kata ya Iramba, ambavyo ni Isanju, Sikiro, Mwiruruma, Mgala na Nyalugoma.
Kibara Stoo.
Anuani ya Posta: 126, Bunda
Simu: 0282621055
Hamishika: 0742163056
Barua Pepe: ded@bundadc.go.tz
Haki Miliki@ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda