Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ilipokea vitabu vya Kiada na Hadithi kwa shule za Sekondari na shule za Awali na Msingi kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), ambapo jumla ya vitabu 371 kwa shule za Sekondari vilipokelewa, na 60,368 kwa shule za Awali na Msingi.
Zoezi la ugawaji wa vitabu lilifanyika siku ya tarehe 10/11/2023 katika shule ya Sekondari Mwibara, iliyopo Kibara Stoo, na jumla ya shule 124 zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ziliweza kugawiwa vitabu hivyo.
Kaimu Afisa Elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Bw. Phinius Ouko alisema jumla ya shule 17 za Sekondari ziligawiwa vitabu vya mchepuo wa Sayansi ambapo kidato cha Nne walipata vitabu 158 kwa somo la Fizikia na Kemia vitabu 126, kwa kidato cha Tatu waligawiwa vitabu 87 kwa somo la Fizikia. Na kwa shule za Awali na Msingi 107, nao waliweza kugawa vitabu 32,240 vya Kiada na vitabu 28,128 vya Hadithi.
“Tunamshukuru sana Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha kuletewa vitabu hivi katika Halmashauri yetu, kwani kupitia vitabu hivi hasa vya madarasa ya Awali na msingi tutapunguza zile KKK mashuleni kwa watoto wetu na kwa upande wa shule za sekondari vitabu hivi vitaongeza motisha kwa walimu na wanafunzi kupenda masomo ya Sayansi”. Alisema Kaimu Afisa Elimu.
Bw. Ouko alisema, tunaiomba serikali pia, ituletee vitabu vya mchepuo wa Kiingereza kwa shule za Awali na Msingi, kwani katika Halmashauri yetu tuna shule ya mchepuo wa Kiingereza ambayo ni Bunda English Medium. Pia tunaomba kuwe na uwiano wa kila mwanafunzi mmoja na kitabu chake shuleni kwa kila somo.
Naye, Mwalimu Zaituni Semvua wa shule ya Msingi Mariwanda A, alisema, anamshukuru Mh. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kuwaletea vitabu hivi na aliipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kupitia Mkurugenzi Mtendaji kwa kufanikisha zoezi hili la ugawaji wa vitabu.
“Zoezi la ugawaji wa vitabu linaenda kuziba sehemu ya mapungufu wa vitabu, ambapo hapo awali kitabu kimoja walikuwa wanatumia wanafunzi Wanne hadi Watano hivyo kupelekea ugumu kwa mwanafunzi kuelewa. Tunashukuru kwa vitabu vya darasa la Nne na la Tano tumeletewa vingi na kwa darasa la Awali hadi la Pili kwa hivi vitabu vya Hadithi vinaenda kupunguza uwingi wa Wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika.” Alisema Mwalimu Semvua.
Naye, Mwalimu wa shule ya Sekondari Mwibara, ambaye ni Mkutubi Bw. Ludonya Lucas alisema, zoezi hili ni zuri kwa serikali na Halmashauri yetu, hivyo aliomba wanapokuwa wanaleta vitabu na kuvigawa wawe wanaleta vitabu vya masomo yote na kwa vidato vyote kuanzia kidato cha Kwanza hadi cha Nne.
“Vitabu hivi vitasaidia kupunguza uhaba tuliokuwa nao hapa shuleni, maana vitabu vya Fizikia na Kemia tulikuwa navyo vichache sana na havitoshelezi” . Alisema Mwalimu Lucas.
Walimu wa shule za Msingi na Sekondari walipongeza zoezi hili la ugawaji wa vitabu vya Kiada na Hadithi, hivyo waliomba Serikali ya awamu ya sita wakishrikiana na Halmashauri waendelee kusisitiza walimu watumie vitabu kwa usahihi kwa kuhakikisha wanafunzi wanahimizwa kuvitumia.
Kibara Stoo.
Anuani ya Posta: 126, Bunda
Simu: 0282621055
Hamishika: 0742163056
Barua Pepe: ded@bundadc.go.tz
Haki Miliki@ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda