Mkurugenzi anayeshughulika na masuala ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe, kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Daktari Rashid Mfaume siku ya tarehe 5/4/2024 alifanya ziara ya kutembelea na kukagua Hospitali ya Wilaya, iliyopo kijiji cha Bukama, Kata ya Nyamuswa.
Daktari Mfaume alisema, lengo la ziara ni kuangalia shughuli za ujenzi wa miradi ya Afya inavyotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, tumekuwa tukiangalia ubora wa huduma za Afya zinazotolewa na changamoto mbalimbali mnazopitia na kuona namna ya kuzitatua changamoto hizo.
Daktari Mfaume, pamoja na timu kutoka OR-TAMISEMI inayoshughulika na masuala ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe, walitembelea na kukagua eneo lote la Hospitali ya Wilaya, pamoja na majengo yote yaliyopo katika eneo hilo, kwa kuangalia changamoto mbalimbali zilizopelekea kutokukamilika kwa majengo mengine katika hospitali, hadi sasa ni majengo matatu tu ambayo yameshakamilika na kuanza kutoa huduma ambayo ni jengo la wagonjwa wa nje (OPD), jengo la dharura (EMD), pamoja na jengo la mionzi.
Mbali na changamoto ya eneo la Hospitali kutokuwa rafiki, lakini masuala ya wizi wa vifaa navyo imepelekea kuchelewa kukamilika kwa ujenzi wa Hospitali, hivyo aliwataka watumishi na wananchi wote kuhakikisha wanakuwa ni walinzi wa vifaa tiba ili waweze kupata huduma iliyo bora, na sio kuiachia kampuni ya ulinzi pekee.
“Hatutavumilia ubadhirifu wa aina yoyote ile katika uhujumu wa vifaa tiba vinavyoletwa katika Hospitali, Mh. Rais amekuwa akizitafuta fedha hizi za kununulia vifaa kwa gharama kubwa sana, lazima tuvilinde na kuvitunza vifaa tiba hivi.” Alisema Daktari Mfaume.
Naye, Mzee wa kijiji cha Bukama, Ndugu Adrew Makaza alisema mbali na kutokukamilika kwa majengo mengine ya Hospitali, tunawashukuru Madaktari kwa huduma nzuri wanazotupatia za matibabu mahali hapa, kutokana na eneo kuwa kubwa tunaomba mtuongezee idadi ya walinzi ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa.
Mtendaji wa Kata ya Nyamuswa, Ndugu Hanington Teikwa Mugabe, alikiri kweli kuwepo na wizi katika Hospitali na tayari wameshachukua hatua katika kuimarisha ulinzi na usalama wa Hospitali kwa kuajiri kampuni ya ulinzi kwa ajili ya kulinda vifaa tiba mahali hapa, hivyo alimuhakikishia Daktari Mfaume suala la wizi wa vifaa tiba halitotokea tena.
Kibara Stoo.
Anuani ya Posta: 126, Bunda
Simu: 0282621055
Hamishika: 0742163056
Barua Pepe: ded@bundadc.go.tz
Haki Miliki@ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda