Kamati ya utekelezaji na usimamizi wa mradi wa kuhimili mabadiliko ya Tabianchi (BCRAP), ikiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Bi. Changwa M. Mkwazu, siku ya tarehe 23/12/2023 ilifanya ziara ya kutembelea na kukagua Mradi wa Samaki uliopo katika Kijiji cha Mchigondo, Kata ya Igundu, pamoja na mashamba darasa mawili ya Mhogo na Mtama yaliyopo katika Kijiji cha Namalebe, Kata ya Chitengule.
Lengo la ziara hiyo ni kukagua miradi hiyo inayotekelezwa chini ya mradi wa kuhimili mabadiliko ya Tabianchi (BCRAP), katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na kuona maendeleo yake na namna wananchi watakavonufaika na miradi hiyo hapo baadae.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo, Mh. Charles Manumbu alimpongeza Mratibu anayesimamia mradi huo Ndugu Johannes Bucha kwa usimamizi wake mzuri katika kuhakikisha miradi yote miwili inaendelea vizuri, ikiwemo mashamba darasa ya Mihogo na Mtama hivyo alimsisitiza kuendelea kutoa elimu zaidi kwa wananchi na kuhakikisha anawasimamia kwa ukaribu ili kuhakikisha miradi inakuwa vizuri hadi kufikia lengo tarajiwa.
Katika ziara hiyo, kamati iliweza kutembelea mabwawa yote ya kufugia Samaki, pamoja na maabara ya kutotoleshea mayai ya Samaki hao, pia, kamati iliweza kupata maelezo kutoka kwa wataalamu mbalimbali wanaousimamia mradi huo katika kuhakikisha wanawatunza Samaki hao na kuhakikisha wanaongezeka.
Hivyohivyo, kwa upande wa kilimo, Mtaalamu wa kilimo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Ndugu,Omben Padon, aliweza kutoa maelezo yake kwa kamati hiyo jinsi ya uanzishwaji wa mashamba darasa hayo na namna wanavyoyasimamia katika kuhakikisha lengo husika linafikiwa kwa wanufaika wa mradi wa kuhimili mabadiliko ya Tabianchi, katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
Halmashauri ya Wilaya ya Bunda inatekeleza mradi wa kuhimili mabadiliko ya Tabianchi, chini ya ufadhili wa Mfuko wa Kimataifa wa kuhimili mabadiliko ya Tabianchi (Adaptation Fund) ambao unasimamiwa na Baraza la Taifa na Usimamizi wa Mazingira(NEMC).
Kibara Stoo.
Anuani ya Posta: 126, Bunda
Simu: 0282621055
Hamishika: 0742163056
Barua Pepe: ded@bundadc.go.tz
Haki Miliki@ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda