Mkuu wa Wilaya ya Bunda Mhe. Lydia Bupilipili amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adam Kigoma Malima katika uzinduzi wa miradi ya vyoo na matanki ya kuvunia maji ya mvua katika halmashauri ya Wilaya ya Bunda. Miradi hiyo imefadhiliwa na shirika lisilo la kiserikali la PCI – Tanzania chini ya ufadhili wa Serikali ya Marekani kupitia Wizara ya Kilimo ya Marekani (USDA). Uzinduzi wa miradi hiyo iliyopo katika Kata 3 za Mugeta, Salama na Ketare umefanyika katika Shule ya Msingi Sanzate iliyopo katika Kata ya Mugeta. Katika uzinduzi huo jumla ya vyoo 6 na matanki 9 ya kuvunia maji yamezinduliwa. Miradi hiyo yenye jumla ya thamani ya Tshs 330,259,576.19 itawanufaisha wanafunzi 7,532 pamoja na walimu 118. Shule za msingi zilizonufaika na mradi huo ni pamoja na Sanzate, Rakana, Tingirima, Salama Kati, Salama ‘A’, Kurusanga, Nyang’aranga, Masaba, Nyaburundu na Kambarage.
Pamoja na ufadhili wa miradi hiyo, shirika la PCI – Tanzania pia limechamgia jumla ya mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa miundombinu ya shule hiyo ya msingi sanzate ikiwa ni kutambua jitihada zinazofanywa na uongozi na pia jamii kwa ujumla katika usimamizi mzuri wa miradi inayotekelezwa shuleni hapo. Akipokea mifuko hiyo ya saruji, Mkuu wa Wilaya ya Bunda Mhe. Lydia Bupilipili aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa, aliwahamasisha wananchi kushiriki katik kuchamgia shughuli za maendeleo ya Elimu ambapo aliweza kuchangisha jumla ya mifuko mingine 100 ya saruji kutoka kwa wananchi waliohudhuria na pia viongozi wa Serikali waliohudhuria uzinduzi huo.
Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Bunda kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara pia aliwaagiza wananchi wote kuhakikisha kunakuwepo na hali ya uendelevu wa miradi yote inayotekelezwa na shirika hilo la PCI – Tanzania ikiwa ni pamoja na mradi wa utoaji wa chakula kwa wanafuzi mara baada ya muda wa wafadhili hao kufikia kikomo. Pia aliwataka viongozi wa Serikali ya Kijiji cha Sanzate kuhakikisha wanasimamia kikamilifu shughuli zote za maendeleo zinazotekelezwa katika kijiji hicho.
Akihitimisha hotuba yake Mkuu wa Wilaya ya Bunda Mhe. Lydia Bupilipili kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Wa Mara Mhe. Adam Kigoma Malima aliushukuru uongozi wa shirika la PCI Tanzania pamoja na walipa kodi wa Marekani kupitia Wizara ya Kilimo (USAID) kwa msaada mkubwa wanaotoa kwa wananchi wa Bunda ikiwa ni kuunga mkono jitihada za Serikali yetu katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Bunda chini ya uongozi wa Rais wetu Mhe. John Pombe Magufuli.
Kibara Stoo.
Anuani ya Posta: 126, Bunda
Simu: 0282621055
Hamishika: 0742163056
Barua Pepe: ded@bundadc.go.tz
Haki Miliki@ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda