Kamati ya siasa ya Wilaya ya Bunda ikiongozwa na Mwenyekiti wa Chama Ndugu Mayaya A. Magesse imepongeza na kuridhishwa na miradi ya kuhimili athari za mabadiliko ya Tabianchi (BCRAP), inayotekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda katika vijiji vya Mchigondo na Mumagunga.
Pongezi hizo zilitolewa siku ya tarehe 16/5/2024 wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua mradi wa ufugaji samaki uliopo katika kijiji cha Mchigondo, Kata ya Igundu ambapo walikagua bwawa la kufugia samaki wazazi, maabara ya kutotoleshea mayai ya samaki na vizimba vya kufugia samaki.
Mratibu wa kuhimili athari za mabadiliko ya Tabianchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Ndugu Johanes Bucha alisema, mbali na ufugaji wa samaki katika kijiji hicho pia wana mradi wa kilimo cha mbogamboga kwa njia ya umwagiliaji wa matone na wameshatenga eneo kwa ajili ya kilimo cha mpunga kwa njia ya umwagiliaji.
Aidha, kamati ilitembelea na kukagua mradi wa ufugaji kuku uliopo katika kijiji cha Mumagunga katika Kata ya Neruma ambapo walijionea maendeleo ya kuku hao. Mwenyekiti wa kamati ya siasa alimuagiza Mratibu wa mradi kuhakikisha anawaletea mashine ya kutotoleshea mayai ya kuku ambapo hadi sasa kuku wameshafikia hatua ya kutaga mayai.
Pia, alimuagiza Mratibu wa mradi kuhakikisha anawajengea uwezo uwezo wafugaji hao wa kuku wa namna ya kutengeneza chakula cha kuku wao wenyewe na sio kuitegemea Halmashauri pekee ili iwawezeshe kupata chakula cha kuku.
“Mradi huu unatakiwa uwe endelevu hivyo inabidi mjifunze namna bora ya kutengeneza chakula wenyewe hata mradi ukifika ukomo muweze kusimama wenyewe kwa ajili ya kujiendeleza na kukuza uchumi wenu,” Alisema Mwenyekiti wa kamati.
Wanufaika wa mradi wa kuhimili athari za mabadiliko ya Tabianchi kutoka Mchigondo na Mumagunga waliwashukuru kamati ya siasa kwa kuja kuwatembelea na waliahidi kuiendeleza miradi yote waliyoletewa katika vijiji vyao.
Pia, walishukuru Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kwa kuwawezesha kuwaletea miradi hiyo katika vijiji vyao kwani imewasaidia wengi na wanaendelea kujifunza kupitia wataalamu mbalimbali kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
Kibara Stoo.
Anuani ya Posta: 126, Bunda
Simu: 0282621055
Hamishika: 0742163056
Barua Pepe: ded@bundadc.go.tz
Haki Miliki@ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda