Katika mkutano wa Baraza la madiwani la kupokea taarifa za robo ya kwanza kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani Mh. Charles Manumbu aliwatunuku watumishi watatu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kwa kazi nzuri ya kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri yaliyopelekea kufikia asilimia 102 kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024.
Hati hizo za pongezi zilitolewa siku ya tarehe 13/11/2024 katika mkutano wa Baraza la madiwani uliofanyika katika ukumbi wa halmashauri uliopo Kibara Stoo.
" Lengo la utoaji wa hati hizi ni kwa ajili ya kuwapa motisha na kutambua juhudi zao katika usimamiaji wa mapato ya Halmashauri vizuri hadi kupelekea kuvuka lengo ambapo katika mwaka wa fedha 2023/2024 Halmashauri ilitarajia kufikia asilimia 100 katika ukusanyaji wa mapato, lakini kutokana na usimamizi na ushirikiano mliounyesha mmeweza kuvuka lengo kwa kufikia asilimia 102." Alisema Mh. Manumbu.
Naye, Katibu Tawala wa Wilaya ya Bunda, Ndugu Salum Khalfan Mtelela alipongeza Baraza la madiwani kwa kutoa hati za pongezi kwa watumishi wa Halmashauri kwa kuweza kusimamia vizuri mapato ya Halmashauri.
Ndugu Mtelela aliwasisitiza waheshimiwa madiwani kuendelea kuhamasisha wananchi kujitokeza siku ya tarehe 27/11/2024 katika kupiga kura za kuchagua viongozi wa serikali za mitaa kwa ngazi za Vijiji na vitongoji.
Katika mkutano huo wa Baraza la madiwani, waheshimiwa madiwani waliweza kuuliza maswali ya papo kwa hapo kwenda kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri na waliweza kupatiwa majibu na ufafanuzi wa maswali yao, pia Baraza lilipokea taarifa mbalimbali zilizowasilishwa kutoka katika taasisi zinazoshirikiana na Halmashauri katika utendaji kazi kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2024/2025.
Kibara Stoo.
Anuani ya Posta: 126, Bunda
Simu: 0282621055
Hamishika: 0742163056
Barua Pepe: ded@bundadc.go.tz
Haki Miliki@ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda