Mkuu wa Wilaya ya Bunda Mh.Dkt Vicent Anney ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kwa kupanda kwa kiwango cha ufaulu Katika matokeo ya mitihani ya kidato cha nne kwa mwaka wa masomo 2024/2025 kutoka asilimia 85 hadi 94% ikilinganishwa na mwaka uliyopita, huku akiwahimiza kuongeza juhudi zaidi katika upande wa elimu ili kuondoa matokeo mabovu katika halmashauri hiyo.
Pongezi hizo amezitoa siku ya tarehe 12/02/2025 katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda uliopo Kibara stoo.
Amesema matokeo ya kidato cha nne kwa mwaka huu yanatia matumaini na yanaonyesha namna gani Halmashauri imeanza kupiga hatua katika upande wa elimu.
"Matokeo ya mwaka huu yanaonyesha njia ni kwa namna gani tumeanza kupiga hatua ukilinganisha na mwaka uliopita hivyo niwasihi kuendelea na kasi hii ili kuendelea kuimarisha zaidi sekta yetu ya elimu katika Halmashauri na Wilaya nzima ya Bunda. "Amesema Dkt Anney
Aidha, Mh.Dk Anney amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kuongeza kasi na juhudi za ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri ili kufikia malengo kama mwaka wa fedha uliopita na kuwasisitiza watumishi wa umma kusimamia majukumu yao kwa kuzingatia kanuni, sheria na utaratibu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Bw. George S. Mbilinyi amesema, ongezeko la ufaulu kwa matokeo ya kidato cha nne limechochewa na uhamasishaji, uboreshwaji wa miundombinu ya elimu pamoja juhudi kubwa na ushirikiano kati ya wataalamu wa elimu kutoka Halmashauri, walimu pamoja na wananchi kwa namna walivyojitoa katika kuchangia mambo mbalimbali ikiwemo chakula kwa wanafunzi shuleni.
Ameongeza kuwa licha ya kuongezeka kwa ufaulu wa matokeo ya kidato cha nne lakini bado kumekuwa na changamoto katika baadhi ya maeneo na wao kama Halmashauri wamekuwa wakiendelea kutafuta utatuzi wa changamoto hizo pamoja na kutoa hamasa ili kuendelea kufanya vizuri zaidi Katika sekta ya elimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
Kibara Stoo.
Anuani ya Posta: 126, Bunda
Simu: 0282621055
Hamishika: 0742163056
Barua Pepe: ded@bundadc.go.tz
Haki Miliki@ 2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda